Afisi ya Rais yatengewa pesa ambazo 'tayari zimeshatumika'
Na CHARLES WASONGA
AFISI ya Rais imetengewa Sh645 milioni katika makadirio ya bajeti ya ziada yaliyowasilishwa bungeni Alhamisi jioni na kiongozi wa wengi Aden Duale.
Fedha hizo zitatumika kufadhili shughuli za operesheni na usafiri wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.
Pesa hizo ni sehemu ya jumla ya Sh163.6 bilioni ambazo wabunge wametakiwa kuidhinisha matumizi yazo kabla ya bajeti kuu kusomwa Juni.
Hii ina maana kuwa Wizara ya Fedha inataka asasi ya bunge kudhinisha pesa ambazo tayari zimetumiwa.
Sh279 milioni kati ya pesa hizo ni za kufadhili shughuli za Ikulu na Sh366 miloni ni za kugharamia shughuli za afisi ya Naibu Rais.
Hatua hiyo ya Wizara ya Fedha kutaka wabunge waidhinishe matumizi ya fedha hizo inajiri wakati ambapo wananchi wamekuwa wakilalamikia hatua ya wabunge kulipwa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000.
Malipo hayo yalianza kuhesabiwa kuanzia Agosti 2018; hatua iliyowezesha kila mmoja wa wabunge 349 na maseneta 67 kupokea jumla ya Sh2.2 milioni mwishoni mwa Aprili.
Katika mgao huo wa fedha kwa Afisi ya Rais, kuna Sh213 milioni iliyotengewa kitengo cha utoaji ushauri kwa serikali ambacho iko chini ya afisi hiyo.
Akosoa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, Kimani Ichung’wa alikosoa hatua ya Wizara ya Fedha kuwasilisha bajeti hiyo kuchelewa wakati ambapo wabunge walikuwa wakijiandaa kwenda likizo ya mwezi mmoja.
“Ni makosa kwa Hazina ya Kitaifa kuwasilisha bajeti ya ziada wakati huu ambapo wabunge wanaenda likizo na wakati ambapo wanachanganua makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020,” akasema Ichung’wa
Mbunge huyo wa Kikuyu alisema Hazina ya Kitaifa ilifanya hivyo kimakusudi kwa sababu inafahamu fika kuhusu kalenda ya bunge.
“Hii ina maana kuwa tutachambua bajeti hii pamoja na makadirio ya bajeti ya kitaifa, kazi ambayo ni nzito mno,” akasema Bw Ichung’wa.
Naye kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa John Mbadi alisema kuwa hatua ya Wizara ya Fedha kuwasilisha bajeti ya ziada kuchelewa ni “njama ya watu fulani kupenye bajeti fulani zenye hila”.
“Naona hapa kuna mpango wa watu fulani kutaka kuhadaa bunge kupitisha bajeti fiche za shughuli ambazo hazina maana yoyote kwa Wakenya bali ni njia yao ya kufyonza pesa za umma,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.