Habari Mseto

Afueni kwa hakimu anayeandamwa na kashfa ya ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI March 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HAKIMU mkuu mahakama ya Thika Stellah Atambo amepata afueni dhidi ya kushtakiwa kwa ufisadi wa Sh2milioni baada ya korti kuzima kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka.

Jaji Chacha Mwita alizima Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga na Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) kumtia nguvuni Bi Atambo na kumshtaki kwa ufisadi.

Jaji Mwita alisema afisa wa polisi Nicodemus Mulinge aliyefika kortini na kupata kibali cha kupekuapekua nyumba ya hakimu huyo hakufichua jina lake kwa hakimu mkazi mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Charles Ondieki mnamo Machi 12, 2025 alipopewa agizo la kumchunguza, kumkamata na kumfikisha kortini Bi Atambo.

Jaji huyo alisema kufichwa kwa jina la mshukiwa na Bw Ondieki kulionyesha kuna njama fiche.

Mawakili Dkt John Khaminwa, Danstan Omari, Shadrack Wambui, Samson Nyaberi na Martina Swiga, wanaomwakilisha, walimweleza Jaji Mwita kwamba EACC inakaidi sheria na Katiba kwa kukiuka Kifungu nambari 157 cha Katiba kinachompa DPP mamlaka ya kumkamata na kufungulia washukiwa mashtaka.

Jaji Mwita alifahamishwa kwamba Sheria nambari 85 ya Sheria za Jinai inampa DPP uhuru wa kuteua wakili wa kuongoza mashtaka.

“Hakuna afisa kutoka afisi ya DPP kuomba kibali cha kupekuapekua nyumba ya Bi Atambo,” Bw Omari alimweleza Jaji Mwita.

Mawakili wa hakimu mkuu Stellah Atambo wakiongozwa na Danstan Omari(kati) katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi. PICHA|RICHARD MUNGUTI

Jaji huyo alielezwa EACC ilijitwika jukumu ambalo halina mashiko kisheria na kujaribu kumtia nguvuni hakimu huyo.

Mahakama ilielezwa EACC haiwezi kutekeleza jukumu ambalo haina.

“EACC haina mamlaka kisheria na nguvu kuendeleza kesi yoyote dhidi ya yeyote. Hii ni jukumu la DPP kwa mujibu wa kifungu nambari 157 cha Katiba,” wakili Samson Nyaberi alieleza hakimu.

Jaji Mwita alipiga breki hatua ya kumtia nguvuni na kumshtaki Bi Atambo na kuamuru kesi hiyo itajwe Juni 10, 2025.

Jaji aliamuru DPP na EACC wajibu madai kwamba EACC haina mamlaka ya kuendeleza kesi yoyote ile.

Mahakama ilielezwa kwamba mawakili watatu walioajiriwa na EACC ni maafisa wa uchunguzi na kamwe hawana mamlaka kisheria kuitetea mamlaka hiyo ya kupambana na ufisadi.

“EACC inaweza kuwasilisha tetesi zake kupitia kwa DPP na kamwe wafanyakazi wake hata kama ni mawakili hawana idhini kisheria kusema chochote kortini. Midomo yao imefumwa,” Bw Omari alieleza mahakama.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Harrison Baraza ataamua Machi 18, 2025 ikiwa mawakili walioajiriwa na EACC wanaweza endeleza kesi mahakamani kama vile mawakili kutoka afisi ya DPP.