Habari Mseto

Afueni kwa wahanga wa uvamizi wa mamba Tana River mradi wa maji ukikamilika

Na STEPHEN ODUOR October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI katika baadhi ya vijiji vya Tana Delta, Kaunti ya Tana River, wamepata afueni baada ya mradi wa kusambaza maji safi maeneo yao kukamilika.

Bi Rehema Adhan, mkazi wa Tarasaa, asema awali walitatizika kuchota maji mtoni kwani walikuwa hatarini kuvamiwa na mamba.

“Kila safari ya mtoni ilikuwa hatari. Nilishuhudia mtoto akivutwa na mamba, na kumbukumbu hiyo ilinifanya niwe na hofu kila mara. Leo maji yanapatikana nyumbani, watoto wako salama na tunaishi kwa amani,” akasema.

Bi Caroline Hadia aeleza kuwa maji ya mfereji yamemwokoa kutokana na maumivu ya mgongo, ambayo alipata kufuatia safari ya kutembea zaidi ya kilomita 12 kila siku kusaka bidhaa hiyo muhimu.

“Nilibeba mitungi mgongoni kwa muda mrefu hadi nikaanza kuugua. Nililazimika kutumia maelfu kwa matibabu. Baadaye nilisukuma mitungi kwa mguu kwa shida. Sasa ninafurahi kuona maji yakiwa karibu nami,” akasema.

Kulingana na Bw Fredrick Kimera, mhandisi katika mradi huo uliofadhiliwa na shirika la Water Trust Fund na serikali ya Kaunti ya Tana River, visima vilivyochimbwa maeneo ya Golbanti na Ziwa Shakababo vimesaidia pia shule na taasisi ambazo hazikuwa na maji.

“Mfumo wa zamani ulikuwa umezeeka na maji yalikuwa na tope. Mfumo huu mpya umeshughulikia suala la ubora wa maji, umeongeza kiwango cha maji, na umeundwa ili kudumu angalau miaka 20 kabla kuhitaji kufanyiwa ukarabati,” alieleza Bw Kimera.

Hadi sasa nyumba 890 zimeunganishwa kwenye mradi huo wa maji huku kazi ya upanuzi ikiendelea.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Maji Tana William Jillo, alisema uharibifu wa miundomsingi na wizi wa mabomba unasalia kuwa changamoto kubwa.

“Wachungaji huvunja mabomba ili mifugo ipate maji. Baadhi ya wakazi huiba mabomba ili kutumia shambani. Matukio haya huongeza gharama za ukarabati na kukatiza huduma,” alieleza.

Bw Jillo alisisitiza umuhimu wa jamii kulinda mradi huo.

“Maji haya ni mali ya wananchi. Wakiyalinda yatawahudumia kwa zaidi ya miongo miwili . Watakaopatikana na vifaa vilivyoibwa watakabiliwa na adhabu kali,” alionya.