Habari Mseto

Afukua kaburi la babake usiku kucha akisaka mifupa

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

PHYLIS MUSASIA na NDUNGU GACHANE

MWANAUME alishangaza wakazi kwa kukesha usiku kucha akifukua kaburi la babake, ili apate mifupa yake ndipo atajirike.

Kwenye kisa hicho kijijini Maseno eneo la Subukia, Nakuru, Patrick Mwangi alifukua kaburi la marehemu babake aliyezikwa miaka 19 iliyopita.

Kulingana na watu wa familia yake, Bw Mwangi alikuwa amewaeleza kuwa kulikuwepo na mtu mmoja katika eneo la Rumuruti kaunti ya Laikipia, aliyemuitisha mifupa hiyo ili aweze kumfanya tajiri na pia kuinuka kibiashara.

“Nilipoamka, kama ilivyo kawaida yangu nilitembea hapa nyumbani kuhakikisha kila kitu kilikuwa sawa. Lakini muda mfupi baadaye, nilishangaa kuona mchanga uliochimbuliwa ukiwa karibu na kaburi la shemeji yangu,” akasema Bi Teresia Mumbi ambaye ni shangaziye Mwangi.

Aliongeza kuwa alisongea na kumkuta Mwangi akiwa ndani ya kaburi hilo huku akiendelea kulichimbua.

“Hakutaka kuzungumza nami nilipomuuliza kuhusu alichokifanya. Majirani walipofika, walimwamuru awache na hapo ndipo alirudia kusema kuwa alifanya hivyo kulingana na masharti aliyopewa,” akasema.

Majirani walisema kuwa, wiki mbili zilizopita, Bw Mwangi alijaribu pia kuchimbua kaburi hilo lakini akakanywa vikali na chifu wa eneo hilo.

“Alinieleza malengo yake yaliomchochea kufanya hivyo na akaomba msamaha kwa wazee wa kijiji hiki,” akasema Chifu Peter Muigai aliyeongeza kuwa Bw Mwangi aliapa kutorudia.

Mwangi hata hivyo aliokolewa kutoka kwa mikono ya watu waliotaka kumuua.

Katika Mahakama ya Murangá kijana alikiri mara tatu kuwa alimuua babake wakizozania papai.

Samuel Kamau Njoroge, 27 kutoka kijiji cha Gituura, viungani mwa mji wa Kenol, alikiri mbele ya Jaji Kanyi Kimondo kwamba alimuua Mzee Bw Nyoike Mwaura alipoteteshwa kwa kuchukua papai shambani.

Bw Kimondo ambaye alishangazwa na jinsi barobaro huyo alivyokiri makosa hayo haraka alienda hatua moja zaidi na kumsomea mashtaka ya mauaji kwa mara ya tatu na tena akakubali kuyatenda.

Ni kutokana na hayo ambapo Jaji Kimondo alimwaamuru ashauriane na wakili wake ambaye hakuwa mahakamani kabla kusomewa mashtaka hayo tena mnamo Oktoba 16 wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo.