Habari Mseto

Ageuza shule kuwa karakana

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WACHIRA MWANGI

MMILIKI wa shule ya kibinafsi katika eneobunge la Mvita, Kaunti ya Mombasa, amelazimika kuigeuza kuwa karakana ya samani baada ya kufungwa kutokana na virusi vya corona.

Bw Shadrack Atik, ambaye ni mmiliki wa Shule ya Msingi ya New Shamy School, alisema alichukua hatua hiyo ili kumwezesha kulipa kodi na kukimu mahitaji ya walimu wake 15.

Alisema alianzisha shule hiyo mwaka wa 1999 na kwa sasa ina wanafunzi 350 kutoka chekechea hadi Darasa la Nane.Hata hivyo, walimu hao wako nyumbani kwani hawezi kumudu kuwalipa mishahara.

“Janga lilitupata bila kutarajia. Lilitangazwa kati ya muhula. La kuridhisha ni kwamba, tulikuwa tushawalipa walimu mishahara yao,” akasema Bw Atik.

Alisema hataki madeni ya shule hiyo kuongezeka hasa kodi, hivyo lazima angetafuta njia mbadala kupata pesa.

“Mpango wangu ni kutafuta pesa kununua jengo ambalo nitaendeshea shule yangu. Hiyo ndiyo hatua pekee itakayoniokolea biashara hii. Tumelazimika kulipa kodi kwa kiasi tu kulingana na kiwango cha fedha tunachopata. Tutafanya hivi hadi shule zitakapofunguliwa mwaka ujao,” akasema.

Alieleza fedha zinazobaki huwa anawalipa walimu wake 15.Mmiliki huyo alisema huenda shule nyingi za kibinafsi zikafungwa kabla ya Januari 2021, kwani nyingi tayari zinakumbwa na changamoto katika ulipaji kodi.

“Kuna ada nyingi ambazo kila mwalimu anahitajika kulipa kwa serikali. Kuna uwezekano mkubwa maafisa wa Halmashauri ya Kitaifa ya Kukusanya Ushuru (KRA) kuanza kutuandama mara tu tutakapofungua shule,” akaongeza.

Maelfu ya walimu katika shule za kibinafsi wameiomba serikali kuwasaidia kifedha ili kujikimu.