Agizo Betika ilipe Sh500,000 kwa aliyecheza na Sh10
NA JOSEPH OPENDA
BETIKA imepoteza rufaa iliyowasilisha mahakamani kupinga kumlipa mcheza kamari David Juma Sh500,000 baada ya ubashiri wake wa mechi nane kutimia sawa.
Bw Juma alitumia Sh10 kubashiri mechi nane kwenye jackpot na kushinda Sh500,000 lakini Betika ilikataa kumlipa pesa hizo ikidai alikosea mechi moja.
Jaji wa Mahakama ya Nakuru Samuel Mohochi alipuuza rufaa ya Betika kuwa haikuwa na msingi wowote mzito wa kuzuia Bw Juma kulipwa hela zake.
Alisema rufaa hiyo iliyowasilishwa mnamo Septemba 12, 2023, haikuwa na uzito wowote.
Betika ilikuwa imekata rufaa kuhusu mahakama ya chini ambayo iliwaamrisha wamlipe Bw Juma hela zake.
“Sioni hoja yoyote yenye mashiko ambayo itafanya niidhinishe rufaa hii. Kwa hivyo, nimeikataa yote kwa kuwa hakuna ushahidi,” akasema Jaji Mohochi.
Betika iliwasilisha rufaa pia ikisema mchakato wa kumtumia Bw Juma pesa zake ulikuwa hauwezi kutimia ndani ya siku 21 ambazo ziliamrishwa na korti.
Uamuzi wa Hakimu Mkaazi wa Nakuru Edward Oboge ndio uliamrisha Betika ilipe pesa hizo ndani ya wiki tatu pekee.
Hata hivyo, Betika ilisema kuchelewa kutuma pesa hizo kulitokana na mchakato wa kufungua akaunti ya benki ambao unachukua muda.
Walidai kuwa kuchelewa kuweka pesa hizo kwenye akaunti kulitokana na mchakato mrefu wa kufungua akaunti za benki na hilo ni suala la usimamizi ambalo hawangeliharakisha.
Tupilia mbali
Hata hivyo, Bw Juma, alipinga rufaa ya Betika akisema ni kama kutumia mahakama vibaya na akataka itupiliwe mbali na kampuni hiyo iangushiwe gharama ya kesi.
Kwenye uamuzi wake, Jaji Mohochi alisema hakukuwa na ushahidi wowote ambao Betika uliwasilisha kortini kuonyesha kuwa benki ndiyo ilikuwa imechelewesha Bw Juma kulipwa pesa zake.
Aidha alisema kuwa iwapo benki ndiyo ingekuwa tatizo, basi pande zote zingefika kortini na kuomba muda wa kufanyika kwa malipo hayo usongeshwe.
Jaji huyo alisema kuwa Mahakama Kuu ina mamlaka ya kukataa rufaa ikiwa hakuna sababu yoyote ya kubatilisha uamuzi wa mahakama ya chini.
Vita kortini kati ya Juma na Betika vilianza baada ya kampuni hiyo kukataa kumlipa Sh500,000 alizokuwa ameshinda.
Pamoja na nduguye Collins Kizito alitumia Sh10 kubashiri mechi nane mnamo Februari 18.
Licha ya kufuatilia malipo hayo, Betika ilikataa kuwajibika ikisisitiza kuwa alikosea mechi moja ilhali haikuwa ukweli.
Mnamo Agosti mahakama ya hakimu iliamrisha Betika imlipe pesa hizo. Bw Juma alisema kuwa alitumia muda wake, pesa na nguvu kuchanganua mechi na inasikitisha kuwa mwishowe alisalitiwa.
Mahakama ilipata Betika na hatia ya kukataa kuheshimu mkataba wake na wachezaji kamari wanaoshinda ikimrejelea Bw Juma.