• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Agizo mabawabu sasa walipwe Sh30,000 kutoka Sh7,000

Agizo mabawabu sasa walipwe Sh30,000 kutoka Sh7,000

NA WANDERI KAMAU

MABAWABU sasa watakuwa wakilipwa Sh30,000 kwenda juu kutoka Sh7,000 kufuatia agizo mpya lililotolewa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Mashirika ya Walinzi Binafsi (PSRA), Bw Fazul Mahamed.

Kulingana na takwimu kutoka kwa PSRA, sekta hiyo inawaajiri zaidi ya Walenya 1.3 milioni, ambao huwa nguzo muhimu katika kudumisha usalama nchini.

Mnamo Jumamosi, Bw Mahamed alisema inasikitisha kuwa walinzi hao wamekuwa wakilipwa mishahara duni, ilhali huwa wanalinda mali ya mabilioni ya pesa.

Alisema kuwa hilo linawezekana, ikizingatiwa sekta hiyo ina thamani ya zaidi ya Sh150 bilioni.

“Inawezekana mabawabu wakalipwa mishahara bora. Imefikia wakati tuzingatie maslahi yao kwani huwa wanatekeleza majukumu muhimu sana ya kiusalama,” akasema Bw Mahamed.

Baada ya shambulio la kigaidi la Westgate mnamo Septemba 2013, serikali ilisema kuwa mabawabu huwa kitengo cha kwanza cha kutoa ulinzi, panapozuka shambulio hatari kama la kigaidi.

Hivyo, ilisisitiza kuhusu umuhimu wa kulainisha na kuiunganisha sekta  hiyo na vitengo vya usalama vya serikali ya kitaifa.

Ni kutokana na hilo ambapo Jumamosi, PSRA ilianza usajili wa mabawabu wote wanaohudumu jijini Nairobi.

Kwenye zoezi hilo, mabawabu wapatao 30,000 walipewa Namba Maalum ya Utambulisho (GFN), kuonyesha kuwa wamesajiliwa ifaavyo na wana leseni ya kuhudumu, kulingana na kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Kuhalalisha Mashirika ya Kusimamia Askari Rungu (PSRA).

Mabawabu wote wataonyesha nambari hiyo wanapokuwa kazini kama ishara ya uthibitisho wao.

Baada ya kusajiliwa, maelezo ya bawabu husika yatawekwa kwenye hifadhidata ya mamlaka hiyo. Hivyo, kila mmoja anaweza kuthibitisha kuhusu ikiwa askari rungu ni halali au la.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi, Bw Adamson Bungei, alisema polisi wote watahitajika kuwatambua askari rungu wanaohudumu katika maeneo wanaokotumwa kudumisha usalama.

“Baada ya likizo ya Pasaka na Ramadhani, tutaketi chini na kamati yangu ya usalama na viongozi wenu ili kuanza mfumo mpya wa ushirikiano jijini Nairobi. Naamini kwamba hakuna mwizi au mhalifu anayeendesha maovu yake bila ya kugunduliwa na askari rungu. Tutaketi chini na kuweka mfumo thabiti wa ushirikiano,” akasema.

Hafla hiyo pia ilikuwa imehudhuriwa na Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Matatu ya abiria 14 yanaswa ikibeba wanafunzi 31!

Muziki unaimarisha ubongo na uwezo wa kukumbuka –...

T L