Agizo mjukuu wa Moi akamatwe kwa kukwepa vikao
NA JOSEPH OPENDA
MAHAKAMA ya Nakuru imetoa kibali cha kukamatwa kwa mjukuu wa aliyekuwa Rais wa pili wa Kenya, Mzee Daniel Toroitich arap Moi ambaye amekuwa akikwepa korti kwa zaidi ya miezi miwili.
Hakimu Mkuu wa Nakuru, Kipkurui Kibellion aliamuru kukamatwa kwa Bw Collins Kibet, kwa kudharau mahakama alipotakiwa afike mbele ya mahakama hiyo ili kuonyesha sababu kwa nini hapaswi kuadhibiwa kwa kudharau mahakama.
Hii ni baada ya kubainika kuwa, mjukuu huyo wa Moi hakuweza kupatikana baada ya kushindwa kuheshimu agizo la mahakama mara nne.
Bw Steve Biko, wakili anayemwakilisha aliyekuwa mke wa Bw Kibet, Gladys Jeruto Tagi, aliambia mahakama kwamba juhudi za kumfikia Bw Kibet kama alivyoagizwa na korti hazikufaulu kwa kuwa haijulikani aliko.
Bw Biko alikuwa ameambia mahakama kwamba Bw Kibet hangeweza kupewa hati ya mahakama Kabarak, kaunti ya Nakuru au katika Kaunti ya Nairobi.
Soma Pia: Majuto ya Mjukuu wa Moi: Collins Kibet sasa atoweka, kesi ya kuhepa malezi ikimuandama