Ahadi hewa nyingine? Uhaba wa mbolea washuhudiwa msimu wa upanzi ukianza Rift Valley
Na BARNABAS BII
UHABA wa mbolea umekumba sehemu nyingi za eneo la North Rift huku wakulima wakiharakisha kununua bidhaa hiyo kwa maandalizi ya msimu wa upanzi.
Wakulima hao Jumatatu walisema uhaba wa pembejeo muhimu za shambani unaweza kuhatarisha utoshelevu wa chakula nchini Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) ikikiri kuwa mahitaji ya pembejeo muhimu za kilimo yameongezeka huku uhaba ukishuhudiwa.
“Kufikia sasa tumesambaza magunia 378,000 ya mbolea kwa msimu wa upanzi lakini kuna mahitaji makubwa ya pembejeo za kilimo hasa katika maeneo yanayolima mahindi katika eneo la North Rith,” Titus Maiyo meneja wa NCPB alisema.
Wakulima wengi katika eneo la North Rift, linalotegemewa kwa chakula nchini wameanza msimu wa upanzi unaoendelea hadi Mei.
Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Wizara ya Kilimo, wakulima 5.5 milioni wamesajiliwa kwa mbolea ya ruzuku ya serikali. Baadhi ya magunia 313, 959 ya mbolea yamesambazwa kwa msimu wa upanzi.
“Magunia 418 267 ya mbolea ya thamani ya Sh790,88 milioni yako katika ghala la NCPB na Kenya National Trading Corporation,” ilisema ripoti hiyo.
“Takriban magunia 314,000 yalichukuliwa na wakulima katika kaunti 23,” ilisema ripoti hiyo.
Kaunti za Uasin Gishu na Trans Nzoia zina salio la magunia 68,236 na 17,071 mtawalia ya mbolea.
“Ni wakulima 4,000 pekee kati ya 10,000 waliosajiliwa katika eneo la North Rift ambao wamepokea mbolea ya ruzuku ya serikali,” alisema Kipkorir Menjo, mkurugenzi wa Chama cha Wakulima Kenya (KFA).
NCPB imeanza usambazaji wa mbolea kwa bei ya Sh2,500 kwa gunia kupitia maduka yake kote nchini. Shughuli za upanzi zimeanza Kusini mwa Rift Valley na Nandi katika eneo la North Rift.
Wauzaji wa reja reja katika sehemu nyingi za eneo la North Rift huuza mbolea kwa zaidi ya Sh6,200 na hivyo kuwagharimu wakulima wanaokimbilia kununua mbolea inayofadhiliwa na serikali katika maghala ya NCPB kote nchini.
Kulingana na Katibu wa Wizara ya Kilimo, Dkt Paul Rono, serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo imepanga kununua takriban magunia milioni 7.5 ya mbolea kwa msimu wa upanzi unaoendelea.
Zaidi ya wafanyabiashara 16,000 wa kilimo wamesajiliwa kufanya kazi na wazalishaji wakuu kuhakikisha mbolea hiyo inasambazwa karibu na wakulima.