Habari Mseto

Ahadi nyingine: Wanajeshi waambiwa watajengewa nyumba mpya 3,000

May 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JOSEPH OPENDA

SERIKALI  imeanzisha mpango ambao utagharimu mabilioni ya pesa ili kujenga nyumba 3,000  katika kambi mbalimbali za  jeshi kote nchini.

Ujenzi wa makazi hayo ni kusaidia kupunguza ukosefu wa nyumba ambao unawakumba wanajeshi na maafisa wa polisi pamoja na idara nyingine za usalama na ulinzi.

Katika mpango huo nyumba za chumba kimoja, vyumba viwili na vitatu, zitajengwa katika kambi hizo za jeshi ambazo ni Lanet (952), Gilgil (697), Nanyuki (788), Mariakani (152) na  Nairobi (500).

Serikali inatarajiwa kutoa ardhi kwa ujenzi wa nyumba hizo pamoja na ufadhili mdogo huku wafadhili wengine wakitoa huduma za kiufundi na pia ufadhili uliosalia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi Aden Duale, nyumba 980 ambazo zitajengwa kwenye mpango huo zitatengewa wanajeshi na familia zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa nyumba hizo katika kambi ya jeshi ya Lanet, Bw Duale alisema kuwa tatizo la ukosefu wa nyumba limekuwa likiwakumba wanajeshi kwa kipindi kirefu na huu ndio wakati wa kulisuluhisha.

“Mradi huu unaonyesha kuwa KDF pia ina wajibu wa kupata suluhu kwa matatizo yanayozonga nchi. Tunalenga kupunguza tatizo la ukosefu wa nyumba miongoni mwa wanajeshi na familia zao,” akasema Bw Duale.

Waziri huyo pia alifichua kuwa wizara hiyo itashirikiana na idara ya nyumba kujenga nyumba 25,000 katika kambi mpya za kijeshi ambazo zimeanzishwa  katika kaunti za Turkana na Marsabit.

“Mpango huu unaoana na ule ambao umeanzishwa na serikali ya makazi ya gharama nafuu. Wanajeshi kando na kutekeleza wajibu wao wa ulinzi,  wanastahili pia kuishi kwenye makazi mazuri,” akaongeza Bw Duale.

Ujenzi wa makazi ya gharama nafuu katika kambi ya Lanet unatarajiwa kuchukua miaka minne na utagharimu Sh4 bilioni.

Katika mpango huo serikali kupitia wizara ya Ulinzi  inatarajiwa kutoa Sh1 bilioni huku kampuni inayotekeleza ujenzi huo kwenye ekari tano za ardhi  ikitoa Sh3.4 bilioni.

Wanajeshi watakaokuwa wakiishi kwenye nyumba hizo watalipa kodi ambazo zitaelekezwa kwa serikali kwa kipindi cha miaka 15 kufidia pesa ambazo zilitumika katika ujenzi huo.