Habari Mseto

Ahukumiwa kifo kwa kuua mwanamke aliyemkataa

July 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOSEPH WANGUI

MWANAUME wa umri wa miaka 34 amehukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuua mwanamke aliyekataa kushiriki mapenzi naye.

Mshtakiwa Daniel Oyondi Moi alimuua Reginah Kiinya nje ya Kituo cha Polisi cha Mweiga mnamo Aprili 29, 2017 katika eneo la Kieni Magharibi, Kaunti ya Nyeri.

Moi alimkatakata kwa panga mwendazake ambaye ni mama wa watoto wanne na kumuua papo hapo.

Baadaye alijisalimisha kwa polisi kuepuka ghadhabu za umati wa watu waliokuwa wakitaka kumwangamiza.

Katika uamuzi wake, Jaji Teresiah Matheka alisema Moi alitekeleza unyama huo huku akidai kuwa mwathiriwa alikuwa kahaba.

Mwathiriwa alikuwa ameachana na mumewe ambaye ni baba ya watoto wake hivyo Moi alitaka kutumia fursa hiyo kumlazimisha kufanya naye mapenzi.

“Mahakama ni sharti itoe onyo kali kwamba mizozo ya ndoa au mapenzi haifai kusuluhishwa kwa kutekeleza mauaji,” akasema Jaji Matheka.

“Mapenzi au masuala ya kifamilia yanafaa kusuluhishwa kwa njia zifaazo na ikiwa suluhisho halitapatikana ondoka uende zako na wala si kudhuru mwenzio,” akaongezea.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, Moi alijitetea kwamba alikasirika alipompigia simu mwendazake na ikapokelewa na mwanaume ambaye hakumfahamu.

“Alijuana na mwathiriwa kwa muda wa mwaka mmoja. Alijua watoto wake na hata dada zake. Alimshambulia mchana wa jua mbele ya dada zake na rafikiye ambaye alikuwa mjamzito. Alimkata mithili ya kuni. Majeraha aliyopata mwendazake, kwa mujibu wa matokeo ya upasuaji, yalikuwa ya kuogofya,” akasilimulia Jaji Matheka.

Ripoti ya uchunguzi iliyowasilishwa na idara ya ukaguzi wa washukiwa, ilionyesha kwamba mshtakiwa ni mzaliwa wa kijiji cha Ebushirikha, Kaunti ya Kakamega.

Ripoti pia ilionyesha kuwa kijijini Moi anatambuliwa kama mtu mwema licha ya kuwa mbugiaji wa mvinyo.

Wanakijiji wakiongozwa na wazee walisema katika ripoti hiyo, kwamba mauaji yanasababisha laana hivyo mshtakiwa anafaa kufungwa gerezani.