Aibu ya viongozi kulaumiana baada ya mkasa wa Dagoretti
Na VALENTINE OBARA
LAWAMA tele zilitokea kati ya viongozi mbalimbali Jumatatu, kuhusu kitengo cha serikali kilicho na mamlaka ya kuhakikisha shule zinajengwa kwa njia salama.
Usimamizi wa eneobunge la Dagoretti linaloongozwa na Bw John Kiarie, Wizara ya Elimu inayosimamiwa na Prof George Magoha, na Serikali ya Kaunti ya Nairobi ikisimamiwa na Gavana Mike Sonko zilimulikwa baada ya Shule ya Precious Talent kuporomoka.Kila kiongozi alijitahidi kujitetea, ijapokuwa baadaye, Naibu Rais William Ruto alitangaza serikali kuu itaanzisha ukaguzi wa miundomsingi ya shule zote nchini.
Bw Kiarie alisema ingawa eneobunge hupokea mgao wa fedha za Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) ambazo zinaweza kutumiwa kujenga shule bora ya umma, hilo halijawezekana katika Wadi ya Ngando kwa kuwa hakuna ardhi ya umma.
Kulingana naye, wawekezaji wa kibinafsi wanaojenga shule maeneo ya mabanda hufanya kadri ya uwezo wao, lakini ni jukumu la idara ya mipango ya ujenzi katika Serikali ya Kaunti kuhakikisha majengo hayo yanafikia ubora unaostahili.
“Hali ya shule kama hii si hapa Dagoretti pekee bali katika kila mtaa wa mabanda. Shule kama hizi ziko katika kila eneo ya nchi,” akasema.
Lakini kupitia kwa taarifa, Bw Sonko alisema ingawa anafahamu kuna utepetevu kiasi fulani katika idara ya kaunti inayosimamia ujenzi, jukumu la kukagua majengo ya shule si la kaunti. Licha ya hayo, alisema amejitolea kuhakikisha kila jengo Nairobi lililojengwa bila kufuata kanuni litabomolewa.
Bw Moses Nyakiongora anayesimamia idara ya kitaifa ya kukagua majengo, alisema kuna wakaguzi wa shule katika Wizara ya Elimu ambao ndio huchunguza ubora wa shule.
Kwingineko, mbunge wa Dagoretti Kusini, Bw John Kiarie alilazimika kupewa ulinzi mkali na polisi kwa muda jana alipozuru Shule ya Precious Talent ambalo liliporomoka na kusababisha vifo vya watoto saba.
Bw Kiarie alikuwa miongoni mwa viongozi wengine wa eneo hilo waliofika kwa haraka mahali pa mkasa kama ilivyo desturi ya viongozi humu nchini. Lakini wananchi wenye ghadhabu waliwakemea viongozi hao kwa kile walichodai ni kuwatelekeza na kujitokeza tu wakati mikasa inapotokea bila kufanya lolote linalowasaidia kwa muda wa kudumu.
“Hawa viongozi hutusahau tunapowahitaji. Sasa wamekuja kutoa ahadi za uongo jinsi walivyozoea. Hatutakubali hilo,” akasema Bw James Okoth, mmoja wa wakazi.