Habari Mseto

Airtel na Telkom sasa zafuata mkondo wa Safaricom, zapandisha bei

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni za mawasiliano ya simu za Airtel na Telkom zimetangaza ongezeko la ada za mawasiliano ya simu kwa senti 30 na 10 kwa huduma za kupiga simu na kutuma ujumbe kwa mfuatano huo.

Hii ni katika utekelezaji wa ongezeko la ushuru lililotangazwa na serikali hivi majuzi.

Kupitia kwa mswada wa fedha 2018, serikali iliongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia 15 kutoka asilimia 10.

Pia serikali iliongeza ushuru wa asilimia 15 wa matumizi ya intaneti.

Hii ina maana kuwa kupigia simu mtumiaji wa Airtel itakuwa ni Sh2.30 ilhali kupigia simu mtumiaji simu asiye mteja wa Airtel itakuwa Sh3.30 kwa dakika moja.

Huduma ya intaneti ya Telkom- Pay-As-You-Go (PAYG) imeongezeka kwa senti 30 kwa MB moja, hivyo ada ya shada hiyo itakuwa ni Sh4.30 kwa MB moja, alisema Aldo Mareuse, Mkurugenzi Mkuu wa Telkom.

Lakini kampuni hizo zilisema kuwa bei ya salio la intaneti (data bundles) litasalia vile vile.

Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Safaricom ilikuwa ya kwanza kutekeleza sheria hiyo mpya ambapo iliongeza ada ya kupiga simu kwa senti 30 na kutuma ujumbe mfupikwa senti.