Habari Mseto

Ajenti wa Mpesa mashakani kwa madai ya kukatalia na Sh392,000 zilizotumwa kwake kimakosa

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA JOSEPH NDUNDA

MFANYABIASHARA ambaye anadaiwa alikataa kurudisha Sh392,000 zilizotumwa kwa namba yake kama ajenti wa Mpesa anakabiliwa na mashtaka ya kukatalia kimakusudi malipo ya kielektroniki kinyume na sheria.

Elizabeth Wanjiru alishtakiwa kwa kukatalia na pesa hizo kimakusudi kinyume na Sehemu 35 ya Sheria ya Makosa ya Kompyuta na Masuala ya Mitandao ya 2018.

Anadaiwa kujiwekea pesa za Frida Wangechi ambazo zilifika kwake kimakosa Januari 11, 2024.

Bi Wangechi ambaye anafanya kazi na Benki ya Equity tawi la Ruai alikuwa anaweka Sh392,000 kama mtaji (float) kwa nambari ya ajenti ya Mpesa ya Bi Wanjiru lakini akajikuta ametuma pesa hizo mara mbili kimakosa, hivyo akatuma Sh784,000 kwa kaunti hiyo.

Alijulisha wafanyakazi wenzake wa ngazi za juu ili kumsaidia kubatilisha na kurudisha pesa za ziada lakini ikashindikana. Bi Wanjiru aliambiwa asitoe pesa hizo kwa kuwa usimamizi ulikuwa umeanzisha mchakato wa kuhusisha Safaricom ili pesa hizo zirudishwe.

Hata hivyo, siku iliyofuata, Safaricom iliambia maafisa wa Equity kwamba hawangeweza kurudisha pesa hizo kwa sababu hakukuwa na chochote kwenye akaunti ya Bi Wanjiru.

Ilidaiwa kwamba Bi Wanjiru pia alizima simu yake na hangeweza kufikika.

Mshukiwa hata hivyo alikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Tito Gesora wa Mahakama ya Makadara.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 au Sh100,000 pesa taslimu.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 5 kabla ya kuanza kusikizwa Julai 8, 2024.

Bi Wangechi na mmoja wa wafanyakazi wenzake wa ngazi za juu waliorodheshwa kama mashahidi.

Video ya CCTV inayomwonyesha Bi Wanjiru akihudumiwa na Bi Wangechi na taarifa ya benki iliyoonyesha kwamba mshukiwa alitoa Sh392,000 zimeorodheshwa kama mambo yatakayotumiwa kama ushahidi.