Habari Mseto

Ajiua kwa madai mumewe anapenda watu wa kwao

November 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

MWANAMKE kutoka eneo la Likoni kaunti ya Mombasa alijitoa uhai baada ya kulumbana na mumewe.Bi Joan Kwamboka, 30, alijinyonga kwa kutumia kipande cha nguo baada ya mgogoro huo kuzuka Jumapili jioni.

Mwili wake ulipatikana umefungwa katika dari ya chumba chake muda mchache baada ya kumtishia mumewe, Bw Elphas Odhiambo, kuwa angejiua.

Mama huyo wa msichana wa miaka tisa, alikuwa amelalama kwa muda kuwa Bw Odhiambo hampi mahitaji yake ya kutosha na kuwa alikuwa anaipendelea familia yake zaidi kumliko yeye.

Wakati wa mzozo huo wa Jumapili, Bi Kwamboka ambaye pia ni mfanyabiashara katika eneo la Likoni alikimbia jikoni na kuchukua kisu ambacho alitishia kumdunga nacho bwanake ambaye wakati huo wote alikuwa aking’ang’ana kushukisha hasira za mkewe.

Aidha, Bw Odhiambo alipoona kuwa hali hiyo inazidi kuwa mbaya alikimbia katika kituo cha polisi cha Likoni kwenda kuitisha usaidizi kutoka kwa maafisa wa usalama ambao aliwajuza kuwa mkewe ametishia kujtoa uhai na alikuwa amejifungia chumbani.

Kulingana na ripoti ya polisi iliondikishwa katika nambari ya matukio ya 32/10/11/2019, Bw Odhiambo alipewa maafisa wa polisi na kuelekea nao nyumbani kwake ili kwenda kumsaidia kutatua shida hiyo.Hata hivyo, walipokuwa njiani, Bw Odhiambo alipokea simu kutoka kwa shemeji yake Bw Haron Nyakundi ambaye alimjulisha kuwa Bi Kwamboka amejitia kitanzi.

“Haron Nyakundi, nduguye mkewe Odhiambo alivunja mlango wa chumba hicho na kupata Bi Kwamboka amejitia kitanzi akitumia nguo. Alimtoa sehemu hiyo kwa haraka na kumkimbiza katika hospitali ya eneo bunge la Likoni ambapo alitangazwa kuwa amefariki,” inasema ripoti ya polisi.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Odhiambo alisema sio mara ya kwanza kwa mke wake kutishia kujitoa uhai wakati wanapokosana.

“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tofauti nyingi kati yetu kwenye ndoa yetu hata wazazi wake walikuwa wamemuita nyumbani ili tuweze kutulia lakini alidinda kwenda,” akasema Bw Odhiambo.

Mwili wa Bi Kwamboka upo katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya mkoa wa Pwani jijini Mombasa ukisubiri kukaguliwa siku ya Jumatano.