Akana kuiba kuku 152
Na RICHARD MUNGUTI
MWANAUME anayeuza bidhaa za reja reja katika soko la Muthurwa Nairobi alishtakiwa kumpora mama kuku 152 wenye thamani ya Sh53,200.
Bw Michael Muia Kamande alikana shtaka hilo la kupokea bidhaa akijifanya anaweza kuzilipia.
Shtaka lilisema mnamo Agosti 8 2020 katika soko la Muthurwa akiwa na nia ya kulaghai alipokea kuku wapatao 152 kutoka kwa Bi Margaret Wangui Thige.
Bw Kamande alidaiwa alimweleza Wangui atamnunulia kuku hao wa kienyeji Sh53,200.
Kiongozi wa mashtaka Bw George Obiri alieleza mahakama baada ya mshtakiwa kupokea kuku hao alitoroka hadi alipokamatwa Jumatano.
Mshtakiwa aliyekuwa na majeraha usoni aliomba hakimu amwachilie kwa dhamana.
Kiongozi wa mashtaka Bw George Obiri hakupinga mshtakiwa akichiliwa kwa dhamana.
Hakimu alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh100,000 na mdhamini mmoja wa kiasi hicho ama alipe pesa tasilimu Sh50,000.
Kesi itatajwa Agosti 31 kutengewa siku ya kusikizwa.