Habari Mseto

Akina baba waua wana wao 4 katika mizozo ya kinyumbani

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VITALIS KIMUTAI na WAIKWA MAINA

MWANAMUME kutoka Kaunti ya Bomet aliwaua wanawe wawili kwa kuwakata kwa panga baada ya kugombana na mkewe kuhusu unga wa ugali.

Mshukiwa anasemekana kuanza ugomvi na mkewe kuhusu pesa alizompa ili anunulie familia unga wa ugali, jambo ambalo inadaiwa mama watoto hakutimiza.

Mkuu wa polisi kaunti ndogo ya Konoin, Bw Alex Shikondi, aliambia Taifa Leo kuwa, mauaji hayo yalitokea Ijumaa usiku katika kijiji cha Shiomo, Cheptalal.

“Kufuatia ugomvi huo, mke alipikia familia chakula kwa haraka na baada ya kula aliondoka na watoto kukimbilia kwa shemeji yake ambaye ni jirani wa hapo karibu,” alisema Bw Shikondi.

Akaongeza: “Mshukiwa anadaiwa kumfuata mama na watoto hadi nyumbani kwa ndugu yake. Akachomoa panga na kuwakatakata watoto wake kabla ya kutoroka.”

Mama watoto aliponea chupuchupu bila majeraha na kutorokea kituo cha polisi kupiga ripoti.

Watoto hao, Boaz Kipkirui, 6, na Elivias Kipkemoi, 4, walikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Cheptalal ambapo iligunduliwa walikuwa wamefariki.

Inadaiwa mshukiwa alikuwa akimshutumu mkewe, ambaye ni mwalimu wa chekechea, kwa kuficha pesa ili azitumie kuanza ndoa na mwanamume mwingine.

Mshukiwa anafanya kibarua katika kiwanda cha majani chai cha Shiomo.

Bw Shikondi alisema polisi wanamsaka huku miili ya watoto hao ikihamishwa mochari ya hospitali ya Kapkatet.

Aua kisha ajitia kitanzi

Katika Kaunti ya Nyandarua, mwanamume mwenye umri wa miaka 32, aliwaua wanawe wawili wa kiume kabla ya kujitoa uhai.

Kelvin Wambui ambaye ni mhudumu wa bodaboda mjini Mirangine, aliwaua wanawe baada ya kujaribu kumuua mkewe wa pili Ijumaa asubuhi. Mamake, Margaret Wambui, alielezea masikitiko kuwa hakuweza kubaini mapema kwamba mwanawe alikuwa akipanga mauaji hayo.

“Mienendo ya mwanangu ilibadilika miezi miwili iliyopita. Alikuwa mtu mchapa kazi, msafi na baba anayewapenda vijana wake. Ghafla, alianza kujitenga na watu huku akijifungia nyumbani kwa muda mrefu,” alisema.

Hali ilidorora Jumanne mkewe wa pili, ambaye alikuwa amemuacha na kurudi kwa wazazi wake, alimshtaki kwa polisi kwa kumtishia maisha.

Kelvin hakuondoka nyumbani Alhamisi baada ya kurudi kutoka kituo cha polisi, hadi Ijumaa asubuhi alipokwenda kazini kwa mkewe na kuzua ugomvi katika soko la Gwa Kiongo.