• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Aliyejichimbia kaburi miaka 17 iliyopita kuzikwa

Aliyejichimbia kaburi miaka 17 iliyopita kuzikwa

Na WAWERU WAIRIMU

MWANAUME wa umri wa miaka 77 aliyejichimbia kaburi na kujiandikia usia wake miaka 17 iliyopita, atazikwa Ijumaa katika eneo la Kambi ya Juu, Kaunti ya Isiolo.

Samson Mwongera alijichimbia kaburi alilokoroga mnamo 2002 akisema kuwa lingetumiwa na yeye au mke wake kwa kutegemea nani ambaye angefariki wa kwanza.

“Kila mtu alishangaa na kulia aliposema anataka kujichimbia kaburi lake,” alisema mjane wake Eunice Ngiri Mwongera.

“Kwanza wazee walikataa ombi lake la kutaka kujichimbia kaburi. Baada ya muda mfupi aliwaendea wazee tena na kuwaeleza kwamba alipanga kuchimba kaburi linalofanana na kabati ambapo yeye nami tungezikwa,” akaelezea Bi Mwongera.

Kaburi hilo la futi tatu lina muundo wa kabati na litatumiwa na watu wawili. Mwili wa mtu wa kwanza kufariki utawekwa chini na kufukiwa halafu jeneza la mtu wa pili litawekwa juu.

Kando ya kaburi hilo kuna nafasi ya kuwezesha jamaa na marafiki kuandika rambirambi zao.

Bi Mwongera alisema mumewe alizungumzia suala la kifo mbele ya familia yake bila uwoga.

Awali alikuwa ameshauri kwamba mchanga usiwekwe juu ya jeneza lake lakini akabadili msimamo huo miezi michache kabla ya kufariki mnamo Julai 10, mwaka huu.

Mwaka mmoja baada ya kutengeneza kaburi lake, mfanyabiashara huyo maarufu aliandika historia yake mwenyewe iliyojumuisha elimu, kazi, ndoa na maradhi yatakayomuua.

Mwongera pia alimwandikia usia mkewe ambao utatosomwa leo mazishini. Pia aliandika usia wa mkewe iwapo angefariki wa kwanza.

Mwumini huyo wa Kanisa la Methodist alifanya kazi katika Mahakama ya Meru kama karani kati ya 1969 na 1976 na baadaye akahamishiwa katika mahakama ya Isiolo alikostaafu.

Wakazi wa eneo hilo waliozungumza na Taifa Leo, walisema kuwa huenda mwendazake angeishi kwa miaka mingi zaidi iwapo asingejichimbia kaburi.

  • Tags

You can share this post!

Madiwani kuamua iwapo referenda itafanyika

Washirika wa Ruto Kakamega sasa wabadili wimbo

adminleo