Aliyekuwa KDF azua kioja kudai makosa aliyoshtakiwa sio yake
AFISA wa zamani wa Jeshi (KDF) alizua kioja mahakamani Jumatano, Julai 30, 2024 alipoeleza makosa anayoshtakiwa nayo sio yake ni ya mtu mwingine.
“Mheshimiwa nimeshangaa sana kusikia eti nimeshiriki ulaghai wa chakula cha Sh4 milioni,” Samuel Ouko Rangwa alimweleza Hakimu Mkuu katika mahakama ya Milimani Bernard Ochoi.
Rangwa aliyestaafu kutoka KDF miaka miwili iliyopita aliambia korti, “nidhamu niliyopata kama afisa wa KDF hainiruhusu nishiriki uhalifu. Haya makosa sio yangu. Mwenyewe asakwe na polisi ”
Rangwa alikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kushiriki uhalifu na kupokea bidhaa za thamani ta Sh4 milioni kwa njia ya ulaghai.
Rangwa alikana kati ya Desemba 6 na 11, 2023, akiwa na watu wengine, walikula njama kumlaghai Caroline Mwoni Amusala bidhaa za Sh4,026,700.
BW Ochoi alielezwa na kiongozi wa mashtaja James Gachoka bidhaa Rangwa alizopokea ni magunia 600 ya mchele,mitungi 500 ya lita 20 kila mmoja ya mafuta ya kupika ya thamani ya Sh4,026,700.
Mahakama iliambiwa Rangwa alimweleza bidhaa hizo zilikuwa za chama cha wadumishao amani almaarufu Kenya Veterans For Peace( KVFP).
Shtaka lilisema Rangwa alijua anandanganya. Rangwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.
Gachoka alipinga akisema Rangwa huzuru mataifa ya kigeni na atatoroka.
Lakini Rangwa alipinga akisema yeye ni mkazi wa Kaunti ya Nyanza na alisafiri nje ya Kenya akienda kudumisha amani Siera Leone na hajawahi safiri tena.
Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu hadi Agosti 13, 2024 kesi itakaposikizwa.