Habari Mseto

Aliyekuwa mhariri wa Taifa Leo kuzikwa Alhamisi

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WANGARI

ALIYEKUWA wakati mmoja Mhariri wa gazeti la Taifa Leo, Bw George Mwangi Migui atazikwa  Alhamisi, Novemba 7, nyumbani kwake eneo la Kamune, Kaunti ya Murang’a.

Kulingana na mpwa wake marehemu, Bi Gladys Wangari aliyezungumza jana na gazeti hili, Bw Migui alifariki kutokana na uvimbe kwenye kichwa baada ya kupatikana akiugua kisukari mapema mwaka huu.

“Alikuwa ameanza kuinama upande mmoja hivyo tukafikiri ni matatizo ya neva. Tulimpeleka hospitalini mapema mwaka huu, ambapo alipatikana na ugonjwa wa kisukari. Hata hivyo, hali yake ilizidi kuzorota na tukampeleka katika hospitali moja Komarock alikofanyiwa uchunguzi wa MRI na kupatikana na uvimbe kichwani,” alisema Bi Wangari.

Alieleza kuwa licha ya kupokea matibabu, afya ya marehemu ilizidi kudhoofika huku wakilazimika kumrejesha hospitalini mara kwa mara. Alikuwa amepangiwa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo kichwani.

Bw Migui aliaga dunia mnamo Ijumaa, Oktoba 25, saa nne kasoro dakika kumi asubuhi, katika Hospitali ya Shallom, akiwa na umri wa miaka 67.

Alifanya kazi na Taifa Leo kwa zaidi ya miongo miwili, kabla ya kustaafu miaka minane iliyopita.

Waliofanya kazi naye walimtaja kuwa mzee mpole, aliyekuwa mwalimu kwa wengi katika chumba cha habari.

“Bw Migui na Onesmus Kilonzo, walinishika mkono na kunionyesha njia katika uanahabari,” aliandika Mhariri wa Habari, Bw Juma Namlola kwenye utangulizi wa riwaya yake, Kinamasi Jangwani.

Ameacha watoto wanne aliojaliwa na marehemu mkewe Bi Lucy Wanjiru Mwangi, ambao ni Mary Njeri, Haron Mbugua, Mercy Wangari na Winnie Wangari.