Habari Mseto

Aliyekuwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza azikwa

July 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

XINHUA na FAUSTINE NGILA

Mwendazake rais wa Burundi Pierre Nkurunziza aliyefariki kutokana na mshtuko wa moyo alizikwa Ijumaa eneo la Gitenga, Burundi ya kati.

Waburudi waliovalia mavazi yenye rangi nyeupe walimuomboleza mwendazake katika uwanja wa Gitega baada ya mwili wake kutolewa hospitalini jimbo la Karusi alipokuwa akitibiwa na kufariki.

Jeneza lililofunikwa bendera ya Burundi lilipelekwa hadi mahali alizikwa.

Rais aliyeapiswa Evariste Ndayishimiye alimsifu mwendazake na kumtaja kuwa mwerevu, mpenda kazi, mzalendo na mnyenyekevu katika habari aliyotoa kwenye sherehe hiyo ya kumsindikisha mwendazake.

“Kifo chako ambacho hakikuwa kinatarajiwa kilikuja kama pigo kubwa kwa wananchi wa Burundi ,” alisema Ndayishimiye.

Denise Nkurunziza mke wa Nkurunziza aliwashukuru watu wote kwa kuleta faraja kwenye familia ya Nkurunziza katika nyakati hizo ngumu.

Alimshukuru Bw Ndayishimiye kwa kumsaidia pamoja na familia yake kabla na baada ya kuchukua ofisi.

Wawakilishi kutoka nchi zingine walihudhuria mazishi hayo akiwemo waziri mkuu wa Tanzania Kasim Majaliwa na Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete alihudhuria mazishi.

Alizaliwa 1964 Burundi Kaskazini jimbo la Ngozi. Alikuwa kiongozi wa jamii ya Hutu na alichaguliwa mwaka wa 2005 na kushinda urais tena 2010 na 2015.