Aliyemtishia ripota wa NMG azuiliwa na polisi
NA CHARLES WANYORO
POLISI mjini Meru wanaendelea kumzuilia mfanyakazi wa kaunti aliyetishia kumdhuru mwanahabari wa Shirika la Nation(NMG), kwa kuandika habari zilizoisawiri serikali ya kaunti ya Meru vibaya mbele ya umma.
Marvin Kimathi maarufu kama Marvo Mzito anadaiwa aliandika ujumbe kwenye ukumbi moja wa Whatsapp, akitoa ufafanuzi jinsi ambavyo yeye na wengine wangemwangamiza mwanahabari huyo, David Muchui.
Katika jumbe kadhaa alizoandika, Bw Kimathi alikuwa akiwarai wenzake wabuni njia za kukabiliana na Bw Muchui kwa kutumia propaganda na kumchukua kama mtu aliyepotoka kimaadili.
Bw Kimathi alikamatwa jana baada ya Mkuu wa Polisi ukanda wa Mashariki, Bi Eunice Kihiko, kuandaa mkutano na wakuu wa polisi wa kaunti.
Baraza la vyombo vya habari mnamo Februari lilikuwa limeandika barua ya malalamishi kwa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet likimtaka achukue hatua kali kuhusu vitisho hivyo dhidi ya Bw Muchui.
Mkuu wa Polisi wa Imenti Kaskazini Robinson Mboloi jana alisema wametuma faili ya kesi hiyo kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma(DPP) ili kupata mwelekeo.