Habari Mseto

Aliyeua mwanamume aliyempata na mkewe kitandani mwake aachiliwa huru

May 23rd, 2024 1 min read

JUDITH CHERONO na RUSHDIE OUDIA

MAHAKAMA ya Kisumu imemwaachilia huru mwanaume aliyemuua mwanaume mwingine aliyemfumania na mke wake kwenye kitanda chao cha ndoa.

C.O.O maarufu kama Japolo alitekeleza mauaji hayo mnamo Disemba 6, 2022 katika mtaa wa Manyatta, Kisumu.

Alimfumania mwanaume huyo Eden Michael Otieno akila uroda na mke wake kisha akamkatakata kwa panga mara kadhaa shingoni.

Japolo, ni jina la Kiluo lenye maana ya anayemuenzi na kumcha Mungu.

Odongo, mhudumu wa bodaboda, akijitetea kortini alisema hakujua kilichojiri kati ya muda alipowafumanaia wawili hao, akisema aligutuka na kugundua alikuwa amejiwasilisha katika kituo cha polisi kwa kumuua mtu.

Ushahidi uliokuwa umetolewa mahakamani ulionyesha alikuwa amemwonya mwanaume huyo akomeshe uhusiano na mkewe mara kadhaa lakini hakusikia onyo hilo.