Habari Mseto

Aliyeua rafikiye wakibishania deni la Sh200 akodolea macho kunyongwa

February 12th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MWANAMUME aliyemuua rafiki yake kwa sababu ya deni la Sh200 sasa anakodolea macho hukumu kali baada ya kupatikana na hatia kwa kosa hilo.

Mahakama Kuu ya Mombasa ilimpata na hatia Mwarua Daniel Masa kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Jaji Anne Ong’injo alipunguza shtaka hilo kutoka kwa mauaji hadi lile la kuua bila kukusudia baada ya kupata kwamba nia ya kuua haikuthibitishwa.

“Kipengee cha nia ya kuua hakijathibitishwa. Mstakiwa ameachiliwa kwa kosa la mauaji lakini amepatikana na hatia kwa kosa la kuua bila kukusudia,” alisema Jaji Ong’injo.

Masa alishtakiwa kwa kosa la mauaji. Alishtakiwa kwa kumuua Jackson Musyoka mnamo Septemba 9, 2018 katika kijiji cha Majimoto huko Lunga Lunga Kaunti ya Kwale.

Kesi ya upande wa mashtaka ilikuwa kwamba Masa alikwenda nyumbani kwa marehemu kudai deni lake la Sh200. Hakumpata ndipo Masa akaamua kuchukua meza kama malipo ya deni lake.

Hata hivyo, wakati Masa alikuwa akiondoka na meza akiwa ameibeba mgongoni, marehemu alifika na kushika meza yake. Hapo ndipo vita vilianza huku kila mtu aking’ang’ania meza hiyo.

Mahakama ilisikia kuwa Masa alichukua mpini wa jembe na kumpiga marehemu kichwani.

Mke wa marehemu aliiambia mahakama kuwa Masa alitumia mpini wa jembe kumpiga marehemu kichwani na usoni.

“Masa alikuwa na mpini wa jembe alipokuja nyumbani kwetu kudai pesa zake,” alisema.

Alisema kuwa juhudi zake za kumpeleka mumewe hospitalini kwa matibabu ziliambulia patupu kwani hakuwa na pesa wakati huo.

“Saa 3 asubuhi, marehemu alianza kuvuja damu mdomoni. Alifariki wakati gari lilifika kumpeleka hospitalini,” alisema shahidi huyo.

Mama wa marehemu pia alitoa ushahidi katika kesi hiyo, akisema alikuta marehemu na Masa wakipigana wakati alisikia mayowe kutoka kwa nyumba ya mtoto wake.

“Mwanangu alikuwa ameanguka chini. Nilisimama kati ya mshtakiwa na marehemu na hapo ndipo vita viliisha. Nilimpokonya mshitakiwa mpini wa jembe na kumfanya atoroke,” alisema.

Ripoti ya upasuaji iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha kuwa marehemu alipata majeraha mabaya kichwani yaliyosababisha kifo chake.

Masa alikana shtaka hilo, lakini alijitetea kwa kuthibitisha kuwa alikwenda nyumbani kwa marehemu kuchukua deni lake.

Deni lilikuwa salio la pesa alizolipa kwa ajili ya taa ya sola ambazo alizirudisha kwa marehemu.

“Nilimsubiri sana lakini nikiwa natoka nilikutana na marehemu akaniuliza kwanini nazungumza na mkewe. Kisha majibizano yakaanza na tukaanza kupigana,” alisema.

Kwa mujibu wa Masa, hakumpiga marehemu bali alianguka kwenye jiwe wakati wa purukushani hizo.

Licha ya kumkuta Masa na hatia, Jaji Ongi’njo alisema mshtakiwa hakuwa na nia ya kumshambulia marehemu na kumjeruhi vibaya mwilini na hata kusababisha kifo chake.

“Kama marehemu asingeshikilia meza na kuanza kuing’ang’ania, vita hivyo visingeweza kutokea. Kwa hiyo mahakama hii inaona kuwa mshtakiwa hakuwa na nia ya kumshambulia marehemu na kumdhuru mwilini na hata kusababisha kifo chake,” alisema jaji huyo.

Mahakama ilibaini kuwa ushahidi uliowasilishwa katika kesi hiyo ulionyesha kuwa Masa hakuwa amepanga kwenda kupigana na Musyoka bali kudai Sh200 zake alipoenda nyumbani kwa marehemu.