• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Kiragu ashikilia yeye ndiye kiongozi wa wachache, vita vya ubabe ndani ya UDA vikiendelea

Kiragu ashikilia yeye ndiye kiongozi wa wachache, vita vya ubabe ndani ya UDA vikiendelea

NA WINNIE ONYANDO

VITA vya ubabe ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) jana viliendelea huku kiongozi wa wachache Anthony Kiragu akishikilia kuwa yeye ndiye kiongozi wa wachache katika bunge la Nairobi.

Akiwahutubia wanahabari muda mchache tu baada ya spika wa kaunti hiyo, Kennedy Ng’ondi kusisitiza kuwa Bw Kiragu ndiye kiongozi wa wachache, diwani huyo alisema kuwa tetesi kuwa aling’olewa mamlakani hazina msingi.

“Niko hapa kama kiongozi wa wachache katika bunge la kaunti ya Nairobi kama ilivyosomwa bungeni na spika wetu. Imebainika kuwa hakuna mkutano rasmi uliofanywa wala hatua rasmi iliyochukuliwa ya kuniondoa madarakani,” akasema Bw Kiragu.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya kuripotiwa kuwa Bw Kiragu na mwenzake Mark Mugambi ambaye ni kiranja wa bunge waliondolewa madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na diwani Waithera Chege.

Wakati uo huo, kizazaa kilizuka katika bunge la kaunti ya Nairobi Jumanne baada ya diwani wa Ngei, Redson Otieno kuvurugana na sagenti waliotaka kumtoa nje ya bunge.

Diwani huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bunge inayosimamia maji alizua ‘vurugu’ bungeni kupinga mchakato wa kumuondoa kwenye wadhifa huo.

Kulingana na diwani huyo, hatua iliyochukuliwa ya kutaka kumuondoa kwenye wadhifa huo ulienda kinyume na sheria.

“Sijaelewa ni kwa nini wanadai kuniondoa kwenye wadhifa huo. Sitakubali kwani lazima mchakato mwafaka ufuatiliwe kabla ya kufikia uamuzi huo,” akasema Bw Otieno.

  • Tags

You can share this post!

Mkurugenzi kizimbani kwa kughushi wosia wa marehemu

Utafiti umegundua washukiwa wengi wa wizi na uhalifu...

T L