Apinga pendekezo la kuondoa neno 'harambee' kutoka kwa nembo ya serikali
Na BENSON MATHEKA
MFANYABIASHARA wa Nairobi, ameomba bunge kutokubali pendekezo la kuondoa neno ‘harambee’ katika nembo rasmi ya serikali ya Kenya; coat of arms.
Bw Solomon Kiore, ambaye ni mtafiti na mtengenezaji wa nembo, alisema ombi la Bw Charles Mangua kwamba neno ‘harambee’ lina mikosi halina msingi na halifai kukubaliwa.
Kwenye ombi lake, Bw Mangua anadai kwamba neno ‘harambee’ limeletea nchi hii mikosi, na linafaa kuondolewa katika nembo ya serikali.
Alidai kwamba “nilifafanuliwa na Mungu kuwa mikosi ambayo imekuwa ikikumba nchi hii ingeweza kuepukwa iwapo neno hilo litaondolewa kutoka nembo ya serikali na nafasi yake kuchukuliwa na neno ‘Kenya’.”
Hata hivyo, Bw Kiore ambaye ameunda vifaa vingi vya serikali vilivyo na nembo hiyo anasema kwamba kazi ya sanaa haiwezi kuchukuliwa kuwa ya kishirikiana alivyodai Bw Mangua.
“Sanaa hutoa maelezo kwa kuzingatia ukweli halisi wa mambo; hasa yanayochangia uwiano na umoja wa jamii kwa kuoanisha turathi za kitaifa za wakati huu na wakati ujao,” anasema Bw Kiore kwenye barua yake kwa bunge kupitia karani wa bunge.
Matumaini na mwelekeo
Anaeleza kwamba kazi ya sanaa katika nembo hiyo inapatia Kenya matumaini na mwelekeo.
“Kote ulimwenguni, nchi zote huwa zinatumia sanaa kueleza na kufafanua thamani yake inayozifanya kudumu, kupata nguvu, matumaini na kujitambulisha kwa uadilifu kama jamii,” anasema Bw Kiore ambaye amewahi kuunda viti vilivyokaliwa na rais wa kwanza na wa pili wa Kenya.
Anaeleza bunge kwamba neno Harambee limekuwa sehemu ya historia ya Kenya na linafaa kuhifadhiwa na kuheshimiwa kwa vizazi vijavyo.
Kulingana na Bw Kiore, kuondoa neno hilo ni sawa na kuvuruga mamlaka ya Kenya kama Jamhuri na kunaweza kusababishia nchi hasara ya mabilioni ya pesa.
“Kwa hivyo, pendekezo la Bw Charles Mangua kuhusisha neno hilo na ushirikina halina msingi. Nembo ya Kenya ni kazi ya sanaa ambayo haiwezi na haifai kuhusishwa na ushirikina. Badala yake inafaa kudumishwa na kuhifadhiwa ilivyo kwa vizazi vijavyo kama turathi ya kitaifa,” anaeleza.
Bw Kiore alikuwa mmoja wa waliotetea kuhifadhiwa kwa nembo la taifa ilivyo wakati wa mdahalo wa kubadilishwa kwa katiba ya Kenya iliyopitishwa 2010.
Baadhi ya watu wakati huo walitaka neno hilo kuondolewa katika nembo la serikali.