• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Arama pabaya kwa ulaghai wa ununuzi wa ardhi

Arama pabaya kwa ulaghai wa ununuzi wa ardhi

NA PETER MBURU

Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama (pichani) anatarajiwa kufika katika Mahakama ya Milimani, Nairobi Jumatatu kufunguliwa mashtaka ya ulaghai katika ununuzi wa ardhi, baada ya kulala seli siku tatu.

Kulingana na mkurugenzi wa mashtaka ya umma Bw Noordin Haji, Mbunge huyo atakumbana na mashtaka yanayohusisha kushirikiana na maafisa wa ardhi kaunti ya Nakuru kutumia njia zisizo za kisheria kupokea shamba.

Bw Arama alikamatwa siku ya Ijumaa saa tatu usiku na zaidi ya maafisa 20 wa tume ya kukabiliana na ufisadi (EACC) na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Railways mjini Nakuru ambapo amekuwa akizuiliwa.

Wafuasi wa Bw Arama waandamana nje ya kituo cha polisi cha Railways mjini Nakuru. Picha/ Peter Mburu

Mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki David Gikaria ambaye alimtembelea tangu alipokamatwa jumapili alisema kuwa juhudi zao za kutaka Bw Arama awachiliwe huru kwa bondi ya polisi ziligonga mwamba.

Bw Gikaria alisema kuwa waliishia kutii amri kwani kulionekana kuwa na mvutano baina ya taasisi za serikali na njama kutoka kwa mtu Fulani mbunge huyo asiwachiliwe huru.

Bw Gikaria alisema kuwa kulikuwa na mpango mbunge huyo ajifanye mgonjwa ili akwepe baridi kali ya seli, lakini kukawa na hofu kuwa mpango huo ungetibuka na kuharibu mambo.

Mfuasi huyu sugu wa mbunge huyo apiga magoti akiwaraia polisi wamwachilie kiongozi wao aliyezuiliwa katika kituo cha polisi cha Railways mjini Nakuru. Picha/ Peter Mburu

“Tumejaribu kuwataka polisi wamwachilie kwa bondi kwa misingi kuwa ni mbunge na hawezi kutoroka lakini wamekataa wakisema atavuruga uchunguzi. Kuna watu walijaribu kumshauri ajiugushe jana ili asilale seli kwa mara ya pili lakini akaamua kulala tu. Hata leo yuko tayari kulala kwa siku ya mwisho hadi kesho atakapowasilishwa kortini,” akasema Bw Gikaria.

“Tumekubali kuwa hawezi kuwachiliwa kwa sababu yoyote ile, amekubali ukweli huo na sasa anasubiri kesho,” Bw Gikaria akasema.

Siku ya Jumapili, baada ya wafuasi wake waliokuwa wamepiga kambi nje ya lango la kituo cha polisi cha Railways anapozuiliwa Bw Arama kukata tamaa, walifanya maandamano na kuvuruga Amani wakiwataka polisi kumwachilia kiongozi wao.

Polisi walinda doria nje ya kituo cha polisi cha Railways mjini Nakuru ambapo mamia ya wafuasi waliandamana. Picha/ Peter Mburu

Makumi ya vijana waliojihami kwa mawe, firimbi na matawi walitishia kuvunja lango la kituo hicho ili waingie kwa nguvu, mbali na kuharibu mali hapo.

“Hatuondoki hapa bila Bw Arama, kwani ameiba nini? Ameua mtu? Hakuna Amani bila mbunge wetu,” wakaimba vijana hao.

Maafisa wa kituo hicho walilazimika kuitisha usaidizi ili kukabiliana nao, kwani walikuwa wakielekea kuingia kituoni kwa nguvu.

Lakini baada ya kuona mitutu ya bunduki na vitoza machozi, vijana hao walipepea kwa usalama wao na hawakurudi tena.

Mbeleni kulikuwa na tuhuma kuwa seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen angemtembelea Bw Arama kituoni lakini hakufika.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria anadaiwa kumtembelea Bw Arama kituoni humo usiku wa manane siku ya Jumamosi.

You can share this post!

Boti mpya la kushughulikia mikasa baharini lazinduliwa

URUSI 2018: Ahadi ya pesa ilivyochochea Nigeria kuiyeyusha...

adminleo