• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Arati afika kortini kwa kesi ya mji wa Keroka

Arati afika kortini kwa kesi ya mji wa Keroka

NA WYCLIFFE NYABERI

GAVANA wa Kaunti ya Kisii Simba Arati ametii agizo la Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Nyamira iliyomtaka afike mbele yake kwa kesi ya mzozo wa mji wa Keroka.

Gavana Arati na Kaimu Katibu wa Serikali ya Kaunti ya Kisii Robert Ombasa na watu wengine, walishtakiwa wiki jana kwamba walikiuka maagizo ya mahakama kuhusu mpaka wa mji wa Keroka.

Kesi kuhusu tuhuma hizo ilifikishwa mahakamani na diwani wa Rigoma Nyambega Gisesa na kuwasilishwa mbele ya Jaji Mugo Kamau.

Kaunti za Kisii na Nyamira zimekuwa zikizozania mji huo unaokua kwa kasi.

Kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo, Bw Gisesa (ambaye wadi yake ya Rigoma iko Kaunti ya Nyamira) aliyoyomea mahakamani na kuiomba iweke wazi mahali mpaka huo uliko.

Aidha, Jaji Kamau kwenye uamuzi wa awali alikuwa ametoa uamuzi wake kuhusu mpaka wa Keroka. Uamuzi huo ulitegemea pakubwa ramani za masoroveya kutoka kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kulingana na ramani hizo, sehemu ambazo awali zilikuwa zinachukuliwa kuwa ziko Kisii, zilionekana kuwa ni za Nyamira.

Hivyo wakati wa kutoa uamuzi, jaji Kamau alisema serikali za kaunti hizo zinafaa kuzingatia kulikowekwa vigingi vya kuonyesha mpaka huo.

Jaji Kamau alisisitiza kuwa hilo pia linafaa kufuatwa katika ukusanyaji wa kodi na mapato mengine kutoka kwa wafanyabiashara.

Lakini Jumapili iliyopita, kulitokea vurumai katika mji huo unaokua kwa kasi baada ya maafisa wa kutekeleza amri za Kaunti ya Nyamira kujaribu kuwapokonya wafanyabiashara miavuli.

Miavuli hiyo ya rangi ya chungwa, ilikuwa imepeanwa na Bw Arati kuwakinga wafanyabiashara na hali mbaya ya hewa.

Aidha Bw Arati alichapisha picha na jina lake katika miavuli hiyo.

Kilichokera maafisa wa Nyamira ni kwamba kiongozi huyo wa Kisii katika kupena miavuli aliwakabidhi baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la chini ambalo katika uamuzi wa majuzi kortini, lilipatikana kuwa la Nyamira.

Kwa kuwa mji huo wa Keroka umegawanywa katikati na barabara kuu ya Kisii-Sotik, wafanyabiashara wa upande mwingine ambao hawakupewa miavuli hiyo walionekana ‘mayatima, hali ambayo ilitajwa kwamba ilichochea moto vurumai hizo.

Ilibidi maafisa wa polisi kutumwa hapo kutuliza joto lililokuwa likipanda.

Kufuatia hayo, Bw Gisesa alirudi tena kortini na kupata maagizo hayo.

“Kwa sababu ya uzito wa suala lililotajwa hapa, kesi hii itatajwa Machi 12, 2024, na washtakiwa wote wafike kortini,” agizo hilo la mahakama lilisema.

Mji wa Keroka ulianza kuzozaniwa pindi ugatuzi ulivyoanza, lakini magavana waanzilishi–James Ongwae (Kisii) na marehemu John Nyagarama (Nyamira)–walielewana kiustarabu kugawanya mji huo jinsi barabara ya lami inavyougawa mji huo.

  • Tags

You can share this post!

Hatua za Ariel Henry kutaka kuyaponda magenge Haiti...

Amerika yawawekea vikwazo wafadhili wa Al-Shabaab

T L