• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ashtakiwa kulaghai wawekezaji Sh19m

Ashtakiwa kulaghai wawekezaji Sh19m

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa kampuni ya kukopesha pesa na muumini katika dhehebu la Akorino alitolewa gerezani Jumanne kujibu mashtaka ya kuwapora wawekezaji zaidi ya Sh19m na kuendeleza huduma za benki bila leseni kutoka Benki kuu ya Kenya (CBK).

Obadiah Macharia Maina, mkurugenzi wa Fedha Micro Investments Limited alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot kwa ulaghai na ukiukaji wa sheria za huduma za benki.

Maina anayetumikia kifungo cha miezi sita alichofungwa na Jaji wa Mahakama kuu kwa kukaidi agizo amrudishie Jenel Anaya Sh1.3 milioni.

Mshtakiwa aliyetolewa katika gereza la Naivasha anapotumikia kifungo alisindikizwa hadi kortini akiwa ametiwa pingu na afisa wa uchunguzi wa jinai.

Mashtaka tisa dhidi ya Maina yalikuwa ya kupokea kutoka kwa watu mbali mbali Sh19,394,102 akiwaeleza watakuwa wanapokea faida ya asili mia nane kila mwezi.

Maina aliomba aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu kwa vile ameshtakiwa tena katika Mahakama ya Eldoret atakapopelekwa wiki hii tena kujibu mashtaka.

Katika kesi iliyompelekea asukumwe jela Mahakama kuu ilikuwa imeamuru mshtakiwa amlipe mlalamishi Bi Anaya Sh1.3m.

Mshtakiwa alieleza mahakama atapelekwa Mahakama kuu ya Eldoret kujibu mashtaka mengine.

Aliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh900,000 ama awasilishe dhamana ya Sh1.8m.

Kesi itatajwa Desemba 18 kutengewa siku ya kusikizwa mwaka ujao.

You can share this post!

Piano ilivyobadilisha maisha yake

‘Uuzaji matunda unalipa kuliko biashara ya...

adminleo