Ashtakiwa kumtenga mtoto na mama yake
Na BENSON MATHEKA
Mwanamke alishtakiwa Jumatatu kwa kumchukua mtoto mwenye umri wa miezi tisa na kumtenga na mama yake.
Bi Elizabeth Lihanda alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Kibera Barabara Ojoo na kukanusha kwamba alitenda kosa hilo kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.
Mahakama iliambiwa kwamba alimtoa mtoto huyo kutoka ulinzi wa mama yake Kaunti ya Busia na kumsafirisha Nairobi. Kwa kufanya hivi, ilidaiwa kwamba alikiuka haki za mtoto huyo za kuwa na mama yake na kumnyima mapenzi ya mzazi.
Bi Lihanda ambaye amekuwa akizuiliwa na polisi kwa wiki mbili wakifanya uchunguzi alidai kwamba ni mama ya mtoto huyo aliyemkabidhi amlee. Aliambia mahakama kwamba kulingana na mila na desturi za jamii anayotoka, mama ya mtoto haruhusiwi kumlea. Hata hivyo, hakufafanua zaidi kwa sababu kesi yake haijaanza kusikilizwa.
“Kulingana na maelezo ya mshtakiwa, ninachukulia kuwa amekana mashtaka aliyosomewa. Utakabidhiwa nakala za taarifa za mashahidi, usome na kujiandaa kwa kesi,” Bi Ojoo alisema.
Mwanamke huyo aliyefahamisha mahakama kwamba ni mfanyabiashara jijini Nairobi aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa kiasi sawa au alipe Sh100,000 pesa taslimu. Kesi yake itasikilizwa Februari 16 mwaka ujao.