• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Ashtakiwa kwa kujifanya mshauri wa sheria afisi ya Rachael Ruto

Ashtakiwa kwa kujifanya mshauri wa sheria afisi ya Rachael Ruto

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAUME ameshtakiwa kwa kujifanya mshauri wa masuala ya sheria katika afisi ya mke wa Rais William Ruto, Bi Rachael Ruto.

Benson Masubo almaarufu Benson Waziri Chacha ambaye 2018 alishtakiwa kwa kujifanya Mbunge Maalum Sabina Chege (akiwa mbunge mwakilishi wa kike Murang’a), alifikishwa kortini mnamo Jumanne, Aprili 2, 2024 akikabiliwa na mashtaka mawili.

Shtaka la kwanza alilokana mbele ya hakimu mkuu Bw Bernard Ochi ni kwamba alijifanya kuwa mwanasheria katika afisi ya Mama Rachel Ruto Machi 21, 2024.

Waziri alikana shtaka la pili la kutoa habari za uwongo kwa afisa wa polisi Peter Njeru Nthiga kwamba alikuwa anaandamwa na gari nambari ya usajili KCU 521D lake Patrick Mwangi Kahuhua.

Waziri alimweleza Bw Nthiga kwamba yeye ni mshauri wa kisheria wa Bi Rachael na kwamba alikuwa anahofia maisha yake kwa sababu ya kuandamwa na gari hilo.

Shtaka lilisema Waziri alimtaka Bw Nthiga atumie vibaya mamlaka na uwezo wake kama afisa wa polisi kumkamata Bw Kahuhua.

Mshtakiwa huyo alidaiwa alijua alikuwa anamdanganya Bw Nthiga.

Waziri aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “anaugua maradhi ya Cancer na tayari amekuwa kipofu.”

“Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana. Nimekuwa kipofu na ninasaidiwa na mpenzi wangu ambaye hunipeleka hospitali na kunirudisha kwa nyumba. Hata nikipewa masharti gani nitayatii,” Waziri alimweleza Bw Ochoi.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka aliyeeleza mahakama kwamba mshtakiwa alitoroka katika kesi aliyoshtakiwa kujifanya mbunge maalum Sabina Chege na kujaribu kumtapeli mbunge marehemu Jakoyo Midiwo Sh100, 000.

Pia alikuwa ameshtakiwa kwa kumlaghai Bw Midiwo Sh20, 000 akijifanya ametumwa na Bi Chege.

  • Tags

You can share this post!

Afueni kwa wake wa pili wakipata idhini kuzika mume

Gachagua amtembelea hospitalini polisi aliyedungwa mishale...

T L