Asingizia ulevi baada ya kuwaua mabinti wake wawili
Na BRIAN OCHARO
MWANAMUME anayedaiwa aliua wanawe wawili kikatili katika Kaunti ya Mombasa, ameshtakiwa kwa makosa mawili ya mauaji.
Inadaiwa kuwa mwanamume huyo aliwaua wanawe kwa kuwadunga kisu kifuani na shingoni wiki iliyopita katika eneo la Mshomoroni.
Wiki iliyopita, Bw John Maina Wango’ombe, 30, alikiri kuwauwa wanawe akisema hakukusudia kwani alikuwa mlevi.
Jana alifikishwa katika Mahakama Kuu ya Mombasa na kushtakiwa kwa makosa ya mauaji ya binti zake wawili mnamo Desemba 6, katika eneo la Mshomoroni.
Kabla ya kusomewa mashtaka, Jaji Njoki Mwangi alimuarifu mshukiwa kuwa hataitajika kujibu mashtaka dhidi yake kwa sasa.
Katika mashtaka ambayo alisomewa, upande wa mshtaka ulidai kuwa mshukiwa aliwaua watoto Angel Wanja na Grace Wangui katika eneo la Calvery, Kaunti Ndogo ya Kisauni.
Jaji alielekeza kuwa Bw Maina apelekwe hospitali kufanyiwa uchunguzi wa akili kabla ya kujibu mashtaka ya mauaji ya wanawe.
Jaji Mwangi pia alielekeza afisa wa usajili katika mahakama ya Mombasa kumpa mshukiwa wakili atakayemsimamia katika kesi hiyo.
Pia, Jaji huyo aliagiza mshukiwa azuiliwe katika gereza la Shimo La Tewa huku ripoti ya uchunguzi wa akili ikisubiriwa.
Akiwa mbele ya mahakama ya Shanzu wiki iliyopita , Maina alikiri kuwaua binti zake wawili lakini alisisitiza kuwa alikuwa mlevi wakati alifanya kosa hilo.
“Ni kweli niliwaua binti zangu, nilikuwa mlevi, nilifahamu kosa langu baada ya kupata tena ufahamu,” aliiambia Hakimu Mwandamizi Mkuu Diana Mochache.
Mtuhumiwa huyo aliiambia mahakama kuwa aliwapiga watoto hao na ratili na kuketi juu ya kibuyu bila kujua yale aliyoyafanya
Lakini hakimu alimshauri Bw Maina kutokubli mashtaka kwani uchunguzi bado unaendelea .
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani baada ya kukaa kizuizini kwa siku saba katika kituo cha polisi cha Nyali huku akisubiri uchunguzi na kiini cha mauaji kama ilivyoombwa na polisi.
Ripoti za polisi za awali zinaonyesha kwamba watoto hao walikuwa wakicheza nje ya nyumba yao wakati baba huyo aliwaita kuwagawia maembe ambazo alinunua.
Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 24.