Askari jela wawili wakamatwa kwa kuficha kokeni chooni
Na LUCY MKANYIKA na MWANGI MUIRURI
WAPELELEZI wamewakamata askari jela wawili baada ya picha za video za kamera ya CCTV kuonyesha wakificha kiasi kikubwa cha kokeni chooni katika Gereza la Manyani.
Maafisa hao waliotambuliwa kuwa ni William Chengo na Boniface Kipkorir walinaswa na kamera za CCTV Jumatatu wakificha dawa hizo za kulevyaĀ katika choo kimojawapo katika gereza la Manyani Maximum Security mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta.
Haya yanajiri huku tayari Kanisa Katoliki likitangaza kuwa litajumuika pamoja na idara za serikali na pia jamii kupambana na janga la utumizi wa mihadarati hapa nchini.
Jumatatu, lilimpa motisha Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i likimtaka kutolegeza kamba katika tangazo lake la Jumapili akiwa katika eneo la Pwani kwamba serikali itawaandama wote wanaojihusisha na biashara ya mihadarati.
Kanisa hilo lilisema kuwa kamati yake kuu ya Kitaifa ya Mapadri wake ndiyo itashirikisha juhudi hizo katika shule na pia katika makongamano mengine ya kijamii.
Haya yalitangazwa na Padri Paul Muriuki ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati kuhusu elimu katika kanisa hilo akihutubu mjini Murang’a.
Bw Muriuki alisema kuwa mradi huo umezinduliwa kwa lengo la kuimarisha masomo na pia kuwaokoa vijana mashinani kutokana na athari za kukwamizwa kimaendeleo na mihadarati.
“Katika juhudi hizo, Kanisa Katoliki likitumia makanisa yake yote hapa nchini litazindua miradi ya spoti na warsha katika jamii ili kuwanoa vijana kimawazo ili wasije wakaangamia katika lindi la mihadarati,” akasema Muriuki.
Padri huyo ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo ya elimu katika Kaunti ya Murang’a alisema kuwa juhudi hizo zitafanikishwa kufuatia ushirikiano wa Shirika la Kupambana na Ulevi holela na Mihadarati (Nacada) na pia serikali za kaunti.
Kizingiti
Alisema kuwa kero ya mihadarati imetambuliwa na Kanisa Katoliki kama kizingiti kikuu kwa uboreshaji wa maisha ya vijana wa hapa nchini.
Hayo yanajiri huku muungano wa wazazi katika shule za Mlima Kenya ukitoa wito kwa serikali ikabiliane na walanguzi wa dawa za kulevya katika eneo hilo ili kuimarisha matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta atoe ilani kali kwa maafisa wa usalama ambao huzembea au husajiliwa na mitandao hiyo ya walanguzi kuwa wataandamwa vikali.
Muungano huo unasema kuwa kuna walanguzi ambao wamekuwa wakiwauzia wanafunzi dawa za kulevya hivyo basi kuwanyima umakinifu wa kushughulika na masomo.
Mwenyekiti wa muungano huo Bw James Maruki alisema kuwa wana majina ya washukiwa kadhaa ambao wako na mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya katika eneo hilo la Mlima Kenya.
Alisema kuwa hali hiyo imemaliza ubabe wa masomo miongoni mwa shule tajika za eneo hilo.
Aidha, alidai kuna baadhi ya maafisa wa polisi wa kanda hiyo ambao hushirikiana na walanguzi hao kiasi cha kutopendekeza hatua zozote zichukuliwe ili kuzima jinamizi hilo.