Habari Mseto

Askofu apendekeza shule za mseto pekee nchini

October 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na STEVE NJUGUNA

Askofu wa dayosisi ya Nyahururu ya kanisa Katoliki anataka shule za wanafunzi wa jinsia moja nchini zifungwe na badala yake kuwe na shule za mseto.

Askofu Joseph Mbatia alisema katika shule za mseto, wasichana na wavulana hushirikiana kujifunza mbinu zinazohitajika maishani.

Kulingana naye, shule za wanafunzi wa jinsia moja hazina manufaa yoyote na ni kizingiti kwa maisha ya baadaye ya uhusiano kati ya wasichana na wavulana.

“Shule hizo huchangia kudorora kwa uhusiano ambapo wasichana na wavulana hukua bila kujua jinsi ya kuhusiana na jinsia nyingine,” askofu Mbatia aliambia Taifa Leo. Alisema shule za wanafunzi wa jinsia moja huzuia wanafunzi kujifunza mambo mengi maishani.

Askofu huyo alisema shule za wanafunzi wa jinsia moja haziwezi kuandaa watu kwa maisha ya ndoa licha ya elimu wanayopokea.

Kulingana na kiongozi huyo wa kanisa, wanaosomea shule za jinsia moja huwa wanatatizika kupata wachumba au hata kuwasiliana na watu wa jinsia tofauti.

“Ni wazi kuwa watu wengi ambao hawakujumuika na watu wa jinsia tofauti wakiwa wa umri mdogo huwa wanapata matatizo kudumisha ndoa zao,” aliongeza.