• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Askofu asusia mazishi ya mama yake mzazi ambaye walikosana

Askofu asusia mazishi ya mama yake mzazi ambaye walikosana

Na DERICK LUVEGA

ASKOFU mmoja Jumapili alikosa kuhudhuria mazishi ya mamaye katika Kaunti ya Vihiga, kutokana na mzozo wa uongozi wa kanisa.

Askofu John Mweresa wa Kanisa la African Israel Nineveh alikosa kuhudhuria mazishi ya mamaye, Sarafina Lung’atso, 79, kutokana na mzozo wa muda mrefu wa kanisa hilo.

Mazishi hayo yalifanyika katika kijiji cha Jebrok, chini ya ulinzi mkali wa polisi, ili kudhibiti taharuki iliyotanda. Kulikuwa na hofu kwamba huenda ghasia zingetokea.

Bi Lung’atso, ambaye alihudumu kama kiongozi wa kanisa alimtaka Askofu Evans Chadiva kuchukua uongozi wake, badala ya Askofu Mweresa, ambaye ni mwanawe.

Mzozo huo umekuwepo kwa muda mrefu, ambapo upeo wake ulikuwa mnamo 2015, wakati ghasia zilitokea katika makazi ya familia hiyo ambapo viongozi watatu wa kanisa waliuawa.

Katika mzozo huo, gari ndogo aina ya Saloon na pikipiki tatu zinazomilikiwa na Bw Mweresa zilichomwa.

Askofu Mweresa alitaka mamake kuzikwa nje ya ardhi ya familia ambako ndiko makao makuu ya kanisa hilo yapo.

Alienda katika mahakama ya Hamisi kupinga kuzikwa kwenye ardhi hiyo, lakini mahakama ikatupilia mbali kesi yake.

You can share this post!

Mama Sarah Obama kuadhimisha umri wa miaka 97

Mbunge apinga pendekezo la chama kipya Pwani

adminleo