• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 2:23 PM
Azimio wakosoa mbinu za serikali kukabiliana na mafuriko

Azimio wakosoa mbinu za serikali kukabiliana na mafuriko

Na BENSON MATHEKA

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya umekosoa mbinu ambazo serikali inatumia kukabiliana na mafuriko ambayo yameua watu zaidi ya 200 na kufurusha zaidi 300,000 kutoka makwao.

Viongozi hao wa upinzani wanaitaka serikali kuheshimu haki ya wanaotimuliwa maeneo hatari kwa mafuriko wakisema mbinu za serikali zinawaongezea mateso huku ikiripotiwa watu watatu wamekufa wakati wa ubomoaji wa makazi kando ya mito ya kaunti ya Nairobi.

Wakisema kwamba serikali ilikosa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mafuriko licha ya kushauriwa mapema na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, viongozi wa Azimio la Umoja One Kenya waliitaka kuwajibika na kusaidia wahanga wote waanze kujenga upya maisha yao.

“Tunataka utawala huu kuchukua hatua za mapema za kulinda maisha wakati onyo linapotolewa na kusaidia jamii zinazoishi maeneo hatari kwa mafuriko kuhamia maeneo salama na kwamba izingatie mikakati ya kusimamia janga,” viongozi hao walisema katika taarifa iliyosomwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Walisema hayo huku serikali ikitangaza Ijumaa sikukuu ya kitaifa ya kupanda miti na kuomboleza waliouawa na mafuriko.

Rais William Ruto alisema siku hiyo itakuwa mwanzo wa mpango mkubwa wa kupanda miti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Muungano huo ulisisitiza kuwa ni jukumu la serikali la kutoa misaada cha chakula, dawa, makao na matibabu kwa wahanga wa mafuriko, wanaotimuliwa makwao.

Serikali imetangaza kuwa kila familia iliyoathiriwa na mafuriko itapokea Sh10,000 kiasi ambacho Azimio inataka kiongezwe hadi Sh100,000 kwa kila jamaa.

“Tulisikia Rais Ruto juzi akitangaza akiwa Mathare kwamba kila familia iliyoathiriwa na mafuriko itapata Sh10,000 huku Sh1 bilioni zikiwa zimetengwa kwa shughuli hiyo. Hiki ni kiasi kidogo ambacho kinatolewa kuchelewa. Kwa familia ambazo zimepoteza kila kitu, kiasi hicho hakitoshi kuziwezesha kuanza maisha upya. Tunataka msaada huo wa kifedha kuongezwa hadi angalau Sh100,000 kwa kila familia,” Bw Musyoka alisema.

Muungano huo unaitaka serikali kuomba msaada wa dharura kusaidia waathiriwa wa mafuriko na kurekebisha miundombinu ambayo imeharibiwa na maji zikiwemo taasisi za masomo.

Walishangazwa na hatua ya serikali ya kukataa kutangaza mafuriko kama janga la kitaifa ili iweze kutumia pesa kwa shughuli hiyo na kuvutia misaada kutoka wahisani na wafadhili wa kimataifa.

“Licha ya mvua kuvuruga shughuli nyingi, utawala wa Kenya Kwanza umekataa kutangaza mafuriko janga la kitaifa iweze kupata usaidizi wa kutosha. Tunaelewa kwamba tangazo kama hilo lingehitaji pesa kutumiwa kutoka hazina ya usaidizi ya nchi. Je, inaweza kuwa hakuna pesa katika hazina hiyo? Na iwapo hakuna pesa, nani alizitumia na kwa shughuli gani? Wakenya wanataka kujua,” ilisema taarifa ya Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Mfanyabiashara ajipata pabaya kwa wizi wa Sh54.7m

Kibarua akiri kuiba njugu karanga

T L