Azma ya Gladys Wanga kugeuza chama kuwa benki
Na BERNARDINE MUTANU
Mwakilishi wa Kike Homabay Gladys Wanga analenga kubadilisha chama cha kina mama eneo la Nyanza kuwa benki.
Chama hicho kilicho na washirika 10,000 na alichokianzisha- Homabay County Women’s Sacco kimekuwa kikishirikiana na Hazina ya Serikali Kuu ya Kuimarisha Maslahi ya Makundi yaliyoachwa nyuma(NGAAF), ambayo kufikia sasa imewapa wanachama hao Sh5.5 milioni kutoka mwaka jana.
NGAAF 2017 iliwapa wanawake hao Sh4 milioni na mwaka huu(Februari) iliwapa Sh1.5 milioni.
Pesa hizo huchukuliwa kama mikopo na wanawake na kuwasaidia katika miradi ya maendeleo. Chama hicho kinalenga ushirika kati yake na Hazina ya Kina Mama(WEF), ushirika ambao ikiwa utafanikiwa utakipa nafasi zaidi ya kuwa benki ya kwanza ya wanawake eneo la Nyanza.
Kulingana na Bi Wanga ambaye ni mlezi wa chama hicho, Sacco hiyo inatathminiwa ili kupitisha pesa za WEF katika Kaunti ya Homabay.