Habari Mseto

Azuiliwa kwa kulangua wanawake kutoka Uganda

January 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MKULIMA kutoka kaunti ya Busia alizuiliwa Jumatano kwa siku 14 kuhojiwa kwa madai ya kuwalangua wanawake kutoka Uganda na kuwaingiza humu nchini.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alisema mshukiwa huyo anakabiliwa na madai mabaya kinyume ya sheria za kimataifa.

Bw Cheruiyot alisema kwamba endapo mshtakiwa atafunguliwa mashtaka hayo bila shaka adhabu ya makosa hayo ni kifungo cha miaka mingi gerezani.

Kiongozi wa mashtaka Bi Annette Wangia , alimweleza hakimu kuwa mshukiwa huyo alitiwa nguvuni kutoka Busia na kuzuiliwa na maafisa wa polisi wa kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU).

“Naomba hii mahakama iamuru mshukiwa huyu azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga ndipo awasaidie maafisa wa polisi wa ATPU na maafisa wa kuchunguza jinai (CID)  kumhoji kuhusiana na visa vya kulangua binadamu,” alisema Bi Wangia.

Mahakama ilifahamishwa polisi wanahitaji muda wa siku 14 ndipo wasafiri Busia  na hata Nairobi kuwahoji mashahidi.

Bi Wangia biashara ya kuwalangua binadamu imekuwa ikiendelezwa kupitia njia za panya lakini polisi wamegudua.

Mahakama ilikubalia ombi la Bi Wangia na kuamuru Bw Okirori azuiliwe kwa muda wa siku 14.