• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Baada ya mafuriko, wakazi sasa wavamiwa na nyoka majumbani mwao

Baada ya mafuriko, wakazi sasa wavamiwa na nyoka majumbani mwao

SHABAN MAKOKHA NA LABAAN SHABAAN

WAKAZI wa Kijiji cha Mudende huko Bunyala, Kaunti ya Busia wanaishi na hofu ya kuvumiwa na nyoka.

Hii ni baada ya wanyama hawa kusombwa na maji hadi nyumbani mwao.

Familia ambazo hazikuhama makazi yalioathiriwa na maji wameripoti kuongezeka kwa nyoka nyumbani.

Bi Florence Akinyi, mmoja wa wakazi, anaeleza kuwa amekutana na nyoka wa aina tofauti kila siku.

“Ni kwa sababu ya neema ya Mungu bado tuko hai. Tumeona nyoka aina ya swila, green mamba, na black mamba…taja zote. Tuna hofu,” alisema Bi Akinyi.

Yeye ni miongoni mwa wakazi ambao wamedinda kuhama hadi sehemu salama licha ya kuathiriwa na mafuriko.

Bi Akinyi na majirani wake wamesema kuwa imebidi wakae nyumbani ili watunze mali yao dhidi ya wezi.

“Kuna watu wanaoingia katika nyumba zilizohamwa na kuiba mali,” alieleza.

Bw Oscar Wambia, mkazi wa Kijiji cha Mudambi alidokeza kuwa ni mara ya kwanza eneo hilo limeshuhudia mafuriko.

“Mashamba yetu, makazi na hata kituo cha polisi cha Mudembe kimemezwa na maji,” alisema Bw Wambia.

Wakazi wana hofu kuwa pindi shule zitafunguliwa juma lijalo, watoto wao hawataweza kuhudhuria masomo.

“Ilivyo sasa hatuwezi kufika sokoni ama kuenda kwa majirani sababu maeneo hayo yamemezwa na maji,” Bw Wambua alieleza.

Bw Charles Okumu ameanza kujenga nyumba ya tatu baada ya nyumba zake mbili kuharibiwa na mafuriko ya muda mrefu.

Mwaka wa 2017, Bw Okumu alijenga makao kijijini Mudembe kwa kima cha Sh350,000.

Nyumba hiyo ilibebwa na maji wakati wa mafuriko ya mwaka wa 2019.

Baadaye aliwekeza katika nyumba nyingine ya gharama ya Sh450,000 ambayo aliamini haitaathiriwa na mafuriko sababu alijenga kwenye mwinuko.

“Nimemaliza akiba yangu yote na sina chochote cha kujengea nyumba nyingine kama mvua itaharibu hii,” alisikitika Bw Okumu.

Wakazi wanaomba serikali kuwaundia vizingiti kwenye ukingo wa Mto Nzoia ili kuzuia hasara inayosababishwa na mafuriko.

Jumla ya familia 786 zimeathiriwa na mvua kubwa huku hali ikitarajiwa kuwa mbaya zaidi mafuriko yanavyoendelea.

  • Tags

You can share this post!

Mume hujisaidia kitandani, nimechoka kufua shuka kila siku!

Mitambo: ‘Kisiagi’ cha uchumi wa ‘kadogoo’...

T L