Habari MsetoSiasa

'Baba' amewasha moto ndani ya Jubilee – Kutuny

August 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Cherangany Joshua Kutuny amepasua mbarika kuwa tangu kufanyika kwa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, mambo yanakwenda mrama katika chama cha Jubilee.

Bw Kutuny ambaye amekuwa akikosoa muafaka huo tangu awali Alhamisi alitoa semi zilizoelekea kumaanisha kuwa wandani wa naibu wa rais William Ruto hawajakuwa na amani tena, kutokana na uwepo wa Bw Odinga mezani.

“Sasa unaona Kipchumba Murkomen anakohoa, (Aden) Duale anakohoa, sasa nikasema wacha nimwage maji ndio hawa watu watulie kidogo, baba (kwa maana ya Bw Odinga) ameleta tabu ndani ya Jubilee,” akasema Bw Kutuny katika kikao cha umma.

Kulingana na semi za mbunge huyo, japo kunao wanaofurahia matunda ya muafaka huo wengine wamebaki na kilio, akitumia lugha ya mafumbo kuwa nyumba ya Jubilee imejaa moshi sasa.

“Hii siasa ni hatari, chakula changu ni sumu kwako na kicheko kwangu ni kilio kwako,” Bw Kutuny akaongeza.

Lakini kuwarejelea Seneta wa Elgeyo Marakwet na mbunge wa Garissa mjini Aden Duale ambao ni viongozi wa wengi katika mabunge yote na ambao pia ni wandani wa Bw Ruto kumeonyesha kuwa japo hakuna anayezungumza, huenda mambo yakawa si shwari.

“Na ndio mimi nakuwa mwangalifu kidogo kuhusiana na 2022,” akasema Kutuny.