• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Baba apongeza wanakijiji waliomuua mwanawe mbakaji

Baba apongeza wanakijiji waliomuua mwanawe mbakaji

Na MWANGI MUIRURI

BABA mzazi katika Kaunti ya Kirinyaga, aliwashangaza wanakijiji wenzake alipowapongeza kwa kumuua mwanawe wa kiume aliyedaiwa kuwabaka wanawake 20 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Kijana huyo aliaga dunia akililia umati huo umpe nafasi ya kubadili mienendo yake, lakini ombi hilo likakataliwa. Hata hivyo alipewa dakika tatu za kutubu dhambi zake, ambapo baada ya kuomba na kusema ameokoka alipigwa hadi akafa kisha maiti yake ikachomwa moto.

Alipojitokeza kutazama mwili wa kijana huyo wa miaka 25, babake aliyejitambulisha kama Samson Magu alipongeza umati uliomuua mwanawe akisema alikuwa amejaribu juu chini kumkanya akomeshe mienendo ya uhalifu lakini akapuuza.

“Huyu ni mtoto wangu wa kuzaa. Anaitwa Peter Mwangi na alikataa masomo 2015 akiwa katika kidato cha pili. Ni vyema mambo yake yameisha hivi kwa kuwa hata mbinguni au ahera, hawezi akasema sikumkanya,” akasema Mzee Magu.

Kijana huyo aliandamwa na vijana, wengi wao wakiwa wahudumu wa bodaboda usiku wa kuamkia jana baada ya kudaiwa kumbaka mwanamke mmoja katika kijiji cha Gathiriku, viungani mwa mji wa Ngurubani na wakampiga kwa vifaa butu hadi akafa kisha wakateketeza mwili wake.

Mzee Magu alisema kuwa mwanawe amekuwa akisakwa lakini huhepa kwa kulala kichakani na pia kuhamahama.

“Alikuwa akilenga wanawake ambao wanamfahamu vyema. Wote walikuwa wakiripoti katika vituo vya polisi na pia kwangu,” akasema babake.

“Mwanangu alifaa kufa na sitaki afisa yeyote wa polisi aandame yeyote kufuatia kisa hiki kwa vile nimeondokewa na aibu,” akasema Bw Magu.

Alifichua kuwa kijana huyo amekuwa akimpiga yeye pia: “Kila mara nikijaribu kumkanya abadili mienendo alikuwa akinipiga. Sio mara moja nimeripoti yeye kwa chifu wetu lakini kwa kuwa hakuwa akitiwa mbaroni, akawa tu akinipiga.”

“Ninatoa mwito kwa wazazi wengine wasiwe wa kuhurumia watoto wao ambao wanajiingiza katika uhalifu. Ukishafanya kazi yako ya malezi bora na upate amekaidi kuwa mtiifu kwa sheria, mila na desturi, mwachilie akumbane na adhabu ya dunia,” akasema.

Chifu wa eneo hilo, Peter Gachoki alieleza kuwa kijana huyo alikuwa msumbufu sana kwa wakazi na akasema amepashwa malalamishi zaidi ya 10 na babake kuhusu visa vya kumpiga.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yakosa kulipa wazee miezi 4 mfululizo

Wazazi wa aliyeaga baada ya kutahiriwa wangali mafichoni

adminleo