Baba aua binti yake kwa kumpata na mpenziwe
Na IAN BYRON
POLISI katika eneo la Uriri, Kaunti ya Migori wanamzuilia mwalimu mkuu wa shule ya upili anayedaiwa kumpiga binti yake, 17, hadi kufa akimtuhumu kushiriki ngono na mvulana wa eneo hilo.
Mshukiwa alitambuliwa kama Abidha Rabet, ambaye ni mwalimu mkuu katika Shule ya Upili ya Mseto ya Ugari.
Shahidi wa kisa hicho cha Alhamisi jioni ambaye hakutaka kutajwa alisema mshukiwa alimpiga pia mpenzi wa marehemu na kumjeruhi vibaya.
“Alimpiga sana mvulana huyo kabla ya kuanza kumchapa binti yake. Alimpiga kwa kifaa butu hadi akapoteza fahamu,” akasema.
Ilidaiwa alimpata binti yake nyumbani kwa mvulana huyo ambaye umri wake haukutambulika mara moja.
Kamanda wa Polisi katika kaunti ndogo ya Migori, Bw Peter Njoroge aliiambia ‘Taifa Jumapili’ kwamba, akiwa mwenye ghadhabu, mshukiwa alianza kumpiga mwanawe kwa mwiko hadi akapoteza fahamu.
Marehemu aliyekuwa katika Kidato cha Nne kabla kuangamia alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Neo Care Centre mjini Migori alikotibiwa.
Hata hivyo, hali yake ilizidi kudorora akahamishwa hadi katika Hospitali ya Rufaa ya Migori.
Alifariki katika hospitali hiyo.
Hata hivyo, wazazi wake waliuchukua mwili wake nyakati za usiku kwenye njama ya kuficha chanzo halisi cha kifo chake.
Kulingana na Bw Njoroge, mshukiwa alishirikiana na jamaa zake kadhaa kuusafirisha mwili huo nyumbani kwake katika Kaunti Ndogo ya Bondo ili kuuzika lakini wakafahamishwa na wananchi.
Walilinasa gari lililokuwa likisafirisha mwili lilipokuwa likikaribia mjini Homa Bay.
“Tulishirikiana na polisi wanaosimamia vizuizi vya barabara mjini Homa Bay, ambapo walifanikiwa kulinasa gari hilo lilipokuwa likijaribu kuelekea Kaunti Ndogo ya Bondo. Walipanga kuuzika mwili huo kisiri,” akasema.
Mkuu huyo alieleza kuwa gari hilo lilikuwa limembeba mamake marehemu na jamaa zake wawili. Waliponaswa, waliwapeleka polisi hadi mahali ambapo mshukiwa alikuwa amejificha.
“Alikuwa mwenye wasiwasi wakati polisi walifika nyumbani kwake. Tushamkamata na tutamfungulia mashtaka ya mauaji mnamo Jumatatu,” akasema.
Bw Njoroge alisema mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Misheni ya St Joseph’s Onbo ukingoja kufanyiwa upasuaji.
Alisema uchunguzi kuhusu kisa hicho unaendelea.