Habari Mseto

Bajeti ya kina mama kujifungua bila malipo kuongezwa

April 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliibua kicheko alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa wanahabari katika Ikulu aliposema kuwa serikali yake itaongeza bajeti ya mpango wa kina mama kujifungua bila malipo kwani wengi wamepata uja uzito kipindi hiki cha corona.

Aliongeza kuwa serikali pia itapiga jeki kupanuliwa kwa hospitali ya kujifungua akina mama ya Pumwani ili iwahudumie kina mama wengi mwaka ujao.

“Najua wakati kama huu mwaka ujao pale Pumwani shughuli zitakuwa nyingi zaidi kwa sababu wakati huu wanaume wengi hushinda nyumbani saa nyingi. Na tutaongea bajeti ya mpango wa akina mama kujifungua bila malipo chini ya ajenda yetu ya afya,” Rais Kenyatta akasema.

Alikuwa akijibu swali kutoka kwa mtangazaji wa Redio Jambo Ghost Mulei ambaye alitaka kujua ikiwa serikali yake ina mpango wa kuelekeza pesa zaidi kwa mpango wa akina mama kujifungua bila malipo “kwani hitaji la huduma hizo litaongezeka.”

“Mheshimiwa Rais wakati huu wa janga la corona ambapo wanaume wengi wanafika nyumbani mapema huenda mimba zikawa nyingi. Je, serikali yako itaongeza bajeti ya mpango huo ili kukidhi mahitaji ya huduma hiyo?” akauliza Bw Mulei.

Rais aliongeza kuwa serikali yake bado ingali na matumaini ya kufikia ajenda nne kuu za maendeleo, ikiwemo afya kwa wote, baada ya janga la corona kudhibitiwa. Nguzo zingine katika ajenda hiyo ni, Utoshelezaji wa Chakula, Ustawishaji wa sekta ya utengenezaji bidhaa na ujenzi wa nyumba 500,000 za gharama nafuu ifikapo 2022.

Katika bajeti ya sasa ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 serikali ilitenga Sh330 milioni kufadhili mpango wa akina mama kujifungua bila katika hospitali za umma.