Habari Mseto

Balala ahakikishia wawekezaji sekta ya utalii wizara inafanya kulihali kuzima moto Tsavo

August 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori Najib Balala amewahakikishia wawekezaji katika sekta hiyo kwamba wizara yake itazima moto unaoendelea kuteketeza mbuga ya kitaifa ya wanyama wa porini Magharibi mwa Tsavo.

Bw Balala alisema makundi ya wataalamu wa zimamoto kutoka vitengo mbalimbali, yanaendeleza na juhudi za kuzima moto huo katika eneo la Murka kwenye mbuga hiyo.

Alisisitiza kuwa moto huo ambao umehatarisha wanyama wa porini utazimwa wakati wowote ule.

Bw Balala alisema makundi ya kuzima moto angani na wale wa nchi kavu wanaendelea kutumia vifaa vya kisasa kuzima moto huo.

“Ningependa kupongeza juhudi za taasisi mbali mbali serikalini na washikadau ambao wamejizatiti kuzima moto katika mbuga ya Tsavo. Ilipofika saa nne usiku wa jana, tulikuwa tumedhibiti moto huo lakini sababu ya upepo mkali, moto huo ukazuka tena,” alieleza Bw Balala kwenye anwani yake ya mtandao wa kijamii Facebook.

Amewapongeza wanaozima moto, wakiongozwa na wanajeshi, vijana wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), kamishna wa kaunti hiyo David Sheldrick, Wildlife Trust, jamii ya eneo hilo, waliojumuishwa kwa mpango wa Kazi Mtaani na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS), kwa juhudi zao kukabiliana na mkasa huo.

“Kesho naibu katibu wa idara ya wanyama wa porini Prof Fred Segor, mwenzake wa shirika la KWS Bw John Waweru na kamishna wa kaunti hiyo watazuru eneo hilo kutathmini mkasa huo,” akaongeza.

Mwishoni mwa wiki jana na wiki hii, moto ulizuka katika mbuga za wanyama wa porini upande wa Tsavo Mashariki na Magharibi na kusababisha hasara kubwa kwenye mazingara ya wanyama hao.

Tangu Mei kumekuwa na mikasa ya moto kwenye mbuga hizo. Ni mikasa ambayo imekuwa ikizua hofu miongoni mwa wakazi kwamba huenda ikasambaa katika vijiji jirani.

Shirika la KWS limekuwa likinyooshea kidole cha lawama wakazi wanaopakana na mbuga hizo kwa kuhusika na mikasa hiyo huku wakionywa dhidi ya uovu huo.

Haya yanajiri huku wawekezaji katika sekta ya Utalii wakimtaka Wizari ya Utalii na Wanyamapori kutangaza mikasa ya moto katika mbuga za kitaifa sehemu ya Pwani kama janga la kitaifa.

Wawekezaji hao pia walimtaka Balala kuanza uchunguzi wa mikasa hiyo wakilitaja kama janga hatari nchini.

Haya yanajiri siku chache baada ya Shirika la Wanyamapori nchini kuonya wakazi wanaopakana na mbuga hizo ikiwemo Tsavo na Chyulu dhidi ya kuwasha moto karibu na mbuga hizo.

Shirika hilo lilihusisha jamii jirani kwa mikasa hiyo.