Habari Mseto

Balala awaonya watalii watundu

August 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Utalii Najib Balala amewaonya watalii wa humu nchini na kuwataka waache utundu na ukosefu wa nidhamu unaosababisha wahatarishe maisha yao kila wanapozuru mbuga za kitaifa kujionea wanyamapori na kufurahia mandhari.

Alitaja kisa cha hivi majuzi ambapo baadhi ya watalii wa humu nchini waliozuru eneo la Maasai Mara walionekana wakihatarisha maisha yao kwa kushuka kutoka kwa gari lao.

“Juzi nimekuwa huko Maasai Mara na tumepata wageni wengi wa hapa nyumbani. Tunanawapongeza Wakenya kwa kuzuru eneo hilo kwa sababu wanapiga jeki na kuimarisha sekta ya utalii. Hata hivyo, wageni wanafaa kuwa na nidhamu; si kusimama ovyo juu ya gari ama kutoka nje. Je, ukiumwa na simba utasemaje?” akasema waziri Balala.

Akiongea Jumatano alipozuru mbuga ya Wanyamapori ya Amboseli, Bw Balala alisema hapingi watalii hao kuzuru mbuga za wanyama na “ninachohimiza ni sharti wafuate taratibu na wawe na nidhamu.”

Bw Balala pia alitaja ukosefu wa nidhamu katika mbuga ya kitaifa ya Nairobi huku akimtaka mkurugenzi mkuu wa idara ya wanyama wa porini kushughulikia swala hilo.

“Hakikisha kuna nidhamu katika mbuga zetu; lazima watalii wakae mbali na wanyama wa porini ili wasihatarishe maisha yao,” alisisitiza waziri.

Wakati huo huo ameonya wahusika wa visa vya kuzuka kwa moto katika mbuga ya kitaifa wanyama wa pori ya Tsavo.

“Tutachukua hatua kali za kisheria kwa wale wanaohusika na uovu huo,” alisisitiza.