Habari Mseto

Balozi asema UAE kamwe haihusiki na sakata ya dhahabu

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

TAIFA la Milki za Uarabuni (UAE) limejitenga na sakata ambapo mtu wa familia ya mfalme wa taifa hilo anaripotiwa kulaghaiwa Sh400 milioni, kwa madai angeuziwa dhahabu.

Balozi wa UAE nchini Khalid Al Mualla amesema kuwa hakuna mahali serikali inahusika na wafanyabiashara wa dhahabu wanaohusika na sakata hiyo Kenya, akisema nchi yake haijafurahishwa kuona jinsi Wakenya wamekuwa wakitumia jumbe mitandaoni kuashiria taifa hilo linatoa amri kwa Kenya.

Ujumbe wa balozi huyo ulikuja wakati madai yanazunguka kuwa mtawala wa Dubai Sheikh Mohammed bin Rashid al Maktoum amekuwa akiipa Kenya presha iachilie dhahabu ambazo inasemekana kuzuilia katika uwanja wa ndege.

Akijibu kuhusu madai kuwa kiongozi huyo wa Dubai aliandikia Kenya barua, alisema “Hakuna barua yoyote. Hakujakuwa na mawasiliano yoyote rasmi kati ya Kenya na UAE.”

Ilikuwa mara ya kwanza kwa balozi huyo kuzungumzia suala hilo, ambalo liliibuka mwezi uliopita.

Alisema suala hilo ni la watu na kampuni binafsi, wala si la uhusiano wa mataifa hayo mawili.

Lakini balozi huyo hakusema ikiwa mtawala huyo wa Dubai amehusika katika biashara hiyo ya kununua dhahabu, na akamruka mwanamume kwa jina Ali Zaindi ambaye anasemekana kupokea pesa kutoka kwa Sheikh al Maktoum, kuwa si wa kutoka UAE na pia kuwa hawezi akawa binamu yake mtawala huyo.

“Kuna yeyote anaweza kuthibitisha kuwa dhahabu hizo zilikuwa zikienda kwa mtawala wa Dubai? Nadhani kuna mtu alikuwa akitaka kuharibu uhusiano baina ya Kenya na UAE ambao uko shwari,” akasema.