Barabara mbovu yatatiza usafiri eneo la Munyu
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa kijiji cha Munyu katika Kaunti ya Kiambu leo Alhamisi wamefunga barabara ya kutoka Thika kuelekea kijiji hicho kwa kile walichokitaja kama ubovu wa barabara hiyo.
Wakazi wenye magari wamesema wanateseka kwa sababu ya pancha kila mara.
“Sisi kama wakazi wa Munyu na sehemu za karibu tunapitia masaibu mengi kwa sababu hatuna barabara maalum. Wahudumu wa matatu wanalazimika kuchukua njia ndefu ya kilomita kumi badala ya tano ili kufika kijiji hicho,” amesema mkazi wa Munyu Peter Maina.
Wakazi hao kwa kauli moja wanaitaka Kaunti ya Kiambu ishirikiane na serikali kuu kuona ya kwamba barabara hii inarekebishwa haraka iwezekanavyo.
Wamesema malori makubwa ya kubeba mawe ya ujenzi kutoka kwenye machimbo ya mawe pia ni chanzo cha kuharibika kwa barabara hiyo.
Kwa zaidi ya muda wa saa tano hakuna gari lolote lililoweza kupita katika barabara hiyo kwa sababu wakazi hao walifunga kwa kujaza mawe barabarani huku wakiasha moto mkubwa pahala hapo.
“Wakati huu mvua inavyonyesha magari mengi hasa malori yanakwama kwa matope na kulazimika kupoteza muda mwingi mahali hapo. Sisi wakazi wa hapa tunataka Kaunti ya Kiambu ifanye haraka kuona ya kwamba barabara hii inarekebishwa mara moja,” akasema Bw Martin Kamau ambaye ni mfanyabiashara eneo hilo.
Wakazi hao wamesema biashara nyingi kwa sasa zimedorora kwa sababu hali ya uchukuzi imekwama kabisa.
Amesema watu walioathirika kabisa ni wahudumu wa matatu na bodaboda.
Wakazi hao pia wanataka hatua hiyo ichukuliwe haraka kwa sababu shule zikifunguliwa wanafunzi wengi watatatizika kutokana na usafiri.
“Wakazi wa eneo hili wanaona ni kama wametengwa kwa sababu hakuna chochote kinachowafaidi katika maisha yao,” akasema Bw Kamau.
Wamesema migodi ya mawe ya ujenzi hapa ndicho kitega uchumi cha Kaunti ya Kiambu lakini wanashangaa ni kwa nini barabara ya kisasa haiwezi jengwa eneo hili.