Habari Mseto

Baraza la Agikuyu sasa lamtaka Rais atangaze msimamo wake kuhusu Ruto

June 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

HUKU hali ikiwa si hali tena ndani ya chama tawala cha Jubilee, kundi ndani ya baraza la jamii ya Agikuyu sasa linamtaka Rais Uhuru Kenyatta kutangaza waziwazi kama bado anamwamini naibu wake, Dkt William Ruto.

Limesema kuwa ikiwa uhusiano wao umedorora kiasi cha kuzua hasira hata katika makongamano ya kidini ambapo Rais mnamo Jumapili iliyopita akiwa katika kongamano la Akorino alidaiwa katika matamshi aliyotoa kwamba alikemea mrengo wa Ruto, basi ukweli uandaliwe mapema “watu wajipange nao.”

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kiama Kia Ma (Baraza la Ukweli) katika Kaunti ya Murang’a, Joseph Munga, suitafahamu ambayo inazingira uhusiano wa Rais na Naibu wake “haitupi manufaa yoyote.”

“Leo hii tunaambiwa Rais hasikizani na Ruto, kesho Rais anatumia lugha chafu na iliyojaa vitisho akisemwa kumlenga Ruto… Wakati wa kuambiana ukweli umefika,” amesema Munga.

Bw Munga amemtaka Rais awe mjasiri kikamilifu na hata akitaka amfute kazi Ruto ikiwa “amejipa ushawishi kwamba Raila Odinga ndiye mfaafu zaidi kupewa wadhifa huo.”

Bw Munga alikuwa akirejelea salamu za maridhiano ambazo ziliwaleta pamoja Kenyatta na Odinga na ambapo ‘utengano’ kati ya Uhuru na Ruto unasemwa kuletwa na ushirika huo wa wawili hao.

“Katiba ya nchi inatoa mikakati ya kumtoa Ruto afisini na mwingine ateuliwe. Hatuwezi tukaishi milele na hali hii ya shaka. Ikiwa Rais ameamua Ruto hafai, basi atekeleze mageuzi ndani ya serikali,” amesema.

Wasiwasi

Alisema kuwa Rais kwa sasa anazidisha sintofahamu Mlima Kenya kupitia siasa zake ambazo mara ni moto na mara zingine ni baridi kuhusu urithi wa 2022.

“Alitwambia Ruto ndiye mrithi wake hadi 2032 kuanzia 2022. Lakini akageuka ghafla na akaanza kuonekana kujitenga na Ruto. Tena leo hii anataka kutuambia ndiye atatuchagulia mrithi ilihali yeye hakuchaguliwa sisi na mtangulizi wake, Mwai Kibaki bali tulijiamlia wenyewe,” akasema.

Hata hivyo, kuna makundi tele ya baraza la wazee Mlima Kenya ambayo yamekuwa yakitoa mchango wao kuhusu hali hii, mengine yakishikilia kuwa yanatambua Rais Kenyatta kama msemaji wao rasmi na ambaye ndiye atawapa mwelekeo wa baadaye kuhusu urithi wa 2022.

Ni hali hiyo ya baraza hili la wazee kuwa na makundi mseto ambayo imekuwa ikikemewa na Rais Kenyatta mara kwa mara hadharani.

Rais hachelei kuhadithia jamii yake ya Agikuyu kila mara anapopata fursa ya kuongea nao katika mikutano ya hadhara na ambapo husimulia kuhusu mkutano alioandaa katika ukumbi wa Bomas mwaka wa 2012 katika harakati zake za kutafuta uungwaji mkono wa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2013.

Husema kuwa aliwaalika wazee wa kijamii kutoka kila eneo la hapa nchini na ambapo aliwataka wawasilishe hoja ambazo angehitajika kupea kipaumbele katika manifesto yake ya kufanya kampeni za uchaguzi huo.

Kila jamii iliyowakilishwa ilitoa baraza lao la wazee na ambao katika mkutano huo msemjaji wa baraza hilo alihitajika kuhutubu.

“Mambo yalikuwa shwari katika awamu hiyo ambapo jamii zingine ziliwasilisha hoja zao kwa utulivu wa umoja. Lakini balaa ilituandama wakati wa baraza la wazee wa Agikuyu uliwadia. Walisimama wazee saba, wote wakizozania kuwakilisha jamii hiyo!” Rais alinung’unika.

Anasema hiyo ilikuwa aibu kubwa kwa jamii ambayo alitazamia kutoa mfano wa umoja kwa wengine katika harakati za kuonyesha walikuwa thabiti katika kumwasilisha yeye kama mgombea wa urais.

“Hiyo ndiyo itikadi yetu ambayo tumebeba hadi wa leo. Katika kila uchaguzi, mirengo hiyo hujitokeza ambapo wazee hao wangetaka kuwe na utengano wa umoja na kuwe na mwakilsihi wa chama cha punda, mbuzi, mbwa….na kila aina ya mrengo wa utengano,” anasema.

Hayo yakiendelea kujitokeza, hali halisi ni kuwa, imebainika, kuna shida kubwa ndani ya Jubilee na mzozo unaotokota utaishia kulipuka hivi karibuni, taabani ukiwa ni uthabiti wa serikali na chama cha Jubilee ambacho kimeiunda.