• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Basi la shule lageuzwa matatu jijini

Basi la shule lageuzwa matatu jijini

Na AMINA WAKO

UCHUNGUZI wa Taifa Jumapili umebaini kuwa basi lililonunuliwa kwa shule moja jijini Nairobi sasa limegeuzwa mali ya mtu binafsi na sasa linatumika katika uchukuzi wa umma jijini.

Basi hilo lenye nambari ya usajili KCE- 129 lilinunuliwa na fedha za Hazina ya eneobunge la Embakasi Kusini kwa Shule ya Upili ya St Steven’s mwaka wa kifedha wa 2014/15, wakati Irshad Sumra ambaye anawania kiti cha eneobunge hilo kwa tiketi ya ODM Aprili 5, 2019 alikuwa akihudumu kama mbunge.

Baada ya kupata dokezo kuwa basi hilo lilikuwa jijini, wanahabari wa Taifa Jumapili walizamia kujua liliko ndipo wakalipata katika soka la Nyangancha, Kaunti ya Kisii ambako lilikuwa limeegeshwa kwa muda wa wiki tatu zilizopita. Basi hilo lilikuwa na rangi na maandishi ya mabasi ya City Shuttle yanayohudumu katika barabara kadhaa Nairobi jinsi Taifa Jumapili ilikuwa imedokezewa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu katika Shule ya Upili ya St Steven’s Zablon Karani amekanusha kwamba basi hilo linatumika katika usafiri wa umma.

“Gari lililetwa juzi na vijana wakaambiwa watoe hiyo rangi ya City Shuttle ili nyingine ipakwe. Hata ukiliangalia, washaanza kutoa rangi hapo mbele,” Taifa Jumapili ikaelezwa mjini Kisii huku ikibainika kwamba gari hilo jana liliondolewa na kupelekwa eneo lisilojulikana.

Wanahabari hata hivyo walijipata pabaya katika soko la Nyangancha baada ya genge lililokuwa likilinda basi lenyewe kuwavamia lilipogundua wamelipiga picha na kutaka kujua waliowatuma. Waliwalazimisha wanahabari kufuta picha walizokuwa wamepiga.

“Mngetuuliza kwanza kabla ya kupiga picha. Hili basi lina utata na si vizuri kulipiga picha ilhali hatuwajui wala waliowatuma,”akasema mtu anayedaiwa kuwa dereva baada ya kushauriana na bosi wake kupitia mazungumzo ya simu.

Alipofikiwa, Bw Sumra alikiri walilinunua basi hilo kimakosa kwa St Steven’s na akasema lilifaa kupokezwa Embakasi Girls lakini likahusika kwenye ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya wengi ndipo likapelekwa kwenye karakarana kutengenezwa.

  • Tags

You can share this post!

Murkomen aitwa DCI kuhusu mabwawa

Polisi ndani baada ya kunaswa wakiiba Heroin ya Sh75 milioni

adminleo