Habari Mseto

BBI: Kufuta kwa kiti cha Mwakilishi wa Kike kwazua tofauti

November 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KAMAU MAICHUHIE

PENDEKEZO la Jopokazi la Maridhiano (BBI) la kufutilia mbali wadhifa wa mwakilishi wa kike limegawanya viongozi wanawake huku wale wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto wakipinga kuondolewa kwa nafasi hiyo kwenye katiba.

BBI inapendekeza kwamba wanawake wachaguliwe kama maseneta katika kaunti zote 47 japo kundi la viongozi wa Inua Mama wanapinga pendekezo hilo ambalo limekumbatiwa kuhakikisha usawa wa kijinsia unaafikiwa.

Aidha pendekezo la kufutiliwa mbali kwa wadhifa huo ulitokana na malalamishi miaka ya nyuma ya baadhi ya viongozi wanaume waliosema kuwa haukuwa ukiwanufaisha raia.

Hivi majuzi wabunge 21 wa Inua Mama waliandaa kikao jijini Nairobi ambapo waliapa kwamba wataongoza kampeni za kupinga BBI wakidai ripoti hiyo inafuta matunda yaliyopatikana chini ya katiba mpya ya 2010.

Wawakilishi wa wanawake Faith Gitau (Nyandarua), Rahab Mukami (Nyeri) na mbunge maalum Cecily Mbarire walidai kwamba wanawake wanaoshikilia wadhifa huo wamekuwa wakitoa mchango wao wakati wa kuandaa bajeti na pia wamekuwa wakitumia pesa kwenye hazina yao kusaidia makundi ya akina mama.

Kwa upande mwingine viongozi wanawake ambao wanaunga ukuruba wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga wanasisitiza kuwa mapendekezo yaliyomo kwenye BBI yanaborosha zaidi maslahi ya wanawake kuliko jinsi ilivyo kwenye katiba ya sasa.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na Naibu Kiongozi wa wengi kwenye Seneti Fatuma Dullo (Seneta wa Isiolo) wanasema BBI inatoa suluhu ya kudumu kwa matatizo yanayowakabili wanawake kwenye masuala ya uongozi.

“Wawakilishi wote wa kike 47 bungeni walikuwa wakipokea fedha za maendeleo kutoka kwa hazina ya kitaifa maarufu kama NGAF na pia kutoa mchango wao kwenye uandaji wa bajeti. BBI inawatupa wanawake kwenye Bunge la Seneti lisilokuwa na nguvu na pia kupuuza hitaji la wanawake kushikilia theluthi mbili za nyadhifa kwenye bunge la kitaifa ambalo limepewa mamlaka zaidi,” akasema Bi Gitau.

Mwanasiasa huyo anasema BBI haijafafanua jinsi kuongezwa kwa idadi ya wabunge itahakikisha wanawake wanashikilia theluthi mbili za nyadhifa hizo.

Bi Mukami naye anasema kuondolewa kwa wadhifa huo kwenye katiba ni hujuma wala si haki kwa wanawake nchini Kenya.

“Manufaa yote ambayo wanawake walikuwa wamepata kwenye katiba ya 2010 sasa yanatokomea kupitia BBI. Wadhifa wa mwakilishi wa kike unafaa kusalia hata wakiamua kuwaongezea wanawake nyadhifa kwenye seneti,” akasema Bi Mukami.

Baadhi ya makundi ya kupigania haki za wanawake pia yamepinga kufutiliwa kwa wadhifa huo, wakitaka hilo lifanyike tu baada ya wanawake kupokezwa theluthi mbili za nyadhifa za uongozi.

Msisitizo

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Crawn Trust Daisy Amdany amesisitiza wadhifa huo usiondolewe na badala yake BBI ijikite katika kuhakikisha wanawake wanajumuishwa serikalini na uongozini.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Shirika la Fida-Kenya Joyce Majiwa pia anashikilia wazo kama la Bi Amdany akisema wadhifa huo uondolewe tu baada ya uchaguzi na pale itakapobainika wanawake wamepata nyadhifa zinazozungumziwa.

“Huenda kuna njama ya kutugeuka ndiyo maana lazima yaliyomo kwenye BBI yatekelezwe kikamilifu kabla ya wadhifa wawakilishi wa wanawake kuondolewa,” akasema Bi Majiwa.